
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameipongeza Kampuni ya Puma Energy Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Ammend kwa kutoa elimu ya usalama barabarani kwa watoto walioko shule za msingi.
Asema mafunzo ya usalama barabarani kwa watoto walioko katika shule za msingi yatasaidia kupunguza ajali za barabarani hususan katika maeneo ambayo mafunzo hayo yametolewa huku akishauri elimu hiyo yatolewe nchi nzima kuongeza uelewa.
Pia, amesisitiza kuwa serikali inaamini kwa kufanya hivyo kitaokolewa kizazi cha sasa na kijqacho kwa kuwa elimu ya matumizi bora ya barabara inaendelea kusambaa.
Chalamila amesema hayo leo Novemba 2, 2023 kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa wanafunzi wa shule za msingi walioshiriki shindano la michoro ya kuelimiisha masuala ya usalama barabarani, iliyofanyika katika Shule ya Msingi Kibugumo, Kigamboni, Dar es Salaam, jana .

Amesema kuwa kupitia mafunzo ya usalama barabarani kwa watoto hususan walioko katika shule za msingi Puma imefanya jambo kubwa katika kuepusha ajali za barabarani ambazo zimekuwa sikiisababishia nchi hasara kubwa kwa kupoteza nguvu kazi na mali.
Chalamila mafunzo ya elimu ya usalama barabarani yaliyotolewa na Puma Energy Tanzania kwa kushirikiana na Ammend katika shule tano ni vyema yakatolewa pia katika shule nyingi zaidi kuwajengea uwelewa watoto wangi wa Dar es Salaam na hata nje ya mkoa huo.
“Serikali ya mkoa (Dar es Salaam) tunaamini kuwa kwa kufanya hivi tunaokoa kizazi cha sasa na kijacho kwa kuwa elimu ya matumizi bora na sahihi ya barabarani inaendelea kusambaa,” amesema.
MKURUGENZI PUMA ENERGY
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, amesema mafunzo yaliyotolewa kwa wanafunzi hao ni utekelezaji wa mpango wa ‘Be road safe Africa) unaotekelezwa na Ammend katika nchi tano za Afrika ambazo ni Zambia, Zimbabwe, Tanzania, Botswana na Ghana.

Amesema kuwanzishwa kwa mpango huo kunatokana na takwimu mbaya za ajali za barabarani ambazo zinasababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.
“Nchini Tanzania pekee Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha Usalama Barabarani kimetoa takwimu zinazoonyesha kutokea kwa vifo 1,545 na majeruhi 2,278 kwa mwaka 20222 kutokana na ajali 1,720 za barabarani.
Fatma akizungumzia kampeni hiyo ya ‘Be Road Safe’ amesema kuwa ni jukwaa muhimu shirikishi linalokuza jamii salama kwa watoto.
“Kupitia mashindano hayo ya kuchora tumeongeza ubunifu na uelewa thabiti wa kanuni za usalama barabarani miongoni mwa wanafunzi na kuongeza ufahamu kwa jamii ya Watanzania.
Amesema tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka 2013 ‘Be Road Safe’ umekuwa mwanga wa matumaini na kwamba ni msingi wa kimkakati wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) wa kampuni hiyo chini ya mpango mkuu wa ‘Be Puma Safe’ ambao pia unajumuisha uwezeshaji wa wananchi hususan vijana.
Hafla hiyo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Kibugumo ilihidhuriwa na wadau mbalimbali akiwemo Mkuu wa Dawati la Elimu ya Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi wa Polisi Michael Deleli, Mkurugenzi wa Shirika la Ammend Simon Kalolo, walimu na wanafunzi kutoka shule zilizoshiriki mafunzo na shindano hilo.
Shule za msingi zilizoshiriki mafunzo na shindano hilo ni Kibugumo, Msewe, Mtambani, Kibasila na Kifuru.