
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa Chakoma, alipokuwa akihitimisha mafunzo ya siku moja ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA kwa wajumbe wa Kamati hiyo Februari 12, 2026, bungeni jijini Dodoma.
Mafunzo hayo ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Kamati Januari 19, 2026 wakati OSHA ilipowasilisha taarifa kuhusu muundo na majukumu yake. Lengo ni kuiwezesha Kamati kuisimamia ipasavyo Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) pamoja na taasisi zilizo chini yake, ikiwemo OSHA.
Chakoma ameipongeza OSHA kwa juhudi zake katika kutoa mafunzo kwa waajiri na wafanyakazi, kufanya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya, pamoja na uchunguzi wa afya za wafanyakazi katika hatua mbalimbali. Amesema mafunzo hayo si muhimu tu kwa maeneo ya kazi, bali yanaweza kutumika hata katika mazingira ya nyumbani kukabiliana na hatari mbalimbali.
Amesisitiza kuwa endapo OSHA itatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, Taifa litaepuka gharama kubwa za kuhudumia majeruhi na wagonjwa wa kazini pamoja na kulipa fidia.
Pamoja na pongezi, Kamati imeitaka OSHA kuwashauri wamiliki wa sehemu za kazi kutumia teknolojia na mitambo ya kisasa iliyosanifiwa kupunguza athari za kiusalama na kiafya, ikitolea mfano wa matumizi salama ya vipando (lift) katika majengo marefu.
Aidha, Kamati imependekeza elimu ya usalama na afya itolewe kwa wabunge wote na makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo wakulima wadogo hususan wanaojishughulisha na kilimo cha tumbaku mkoani Tabora.
Mjumbe wa Kamati, Katani Ahmad Katani, amesema anatamani kuona OSHA ikitoa elimu kila mahali kutokana na umuhimu wake, huku Mariam Kisangi akisisitiza haja ya kuendelezwa kwa mafunzo kama hayo kwa manufaa ya wabunge na jamii kwa ujumla.
OSHA ni taasisi iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, yenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, pamoja na kutoa elimu ya usalama na afya kwa waajiri, wafanyakazi na umma.







