×

Simba hasira zote kwa Namungo kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar

KAIMU Kocha Mkuu wa Simba, Daniel Cadena, amefanya kikao na wachezaji wake na kumuahidi kupata matokeo mazuri ya ushindi katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara watakaocheza dhidi ya Namungo FC.

Hiyo ni baada ya kutoka kufungwa mabao 5-1 katika Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga iliyochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Simba inatarajiwa kuikaribisha Namungo katika mchezo huo wa ligi, utakaopigwa leo Alhamisi saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Akizungumza na Spoti Xtra, Cadena alisema kuwa kabla ya kuanza mazoezi ya juzi Jumanne jioni kwenye Uwanja wa Simba, Bunju nje kidogo ya Dar, alifanya kikao na wachezaji wake akiwataka kusahau matokeo yaliyopita na badala yake kujipanga na michezo ijayo ya ligi kwa kuanzia dhidi ya Namungo.

Cadena alisema kuwa mara baada ya kikao hicho, wachezaji wamemuahidi kurejea kivingine katika mchezo dhidi ya Namungo kwa ushindi utakaorejesha furaha za mashabiki wao.

“Niwatake mashabiki wajitokeze kwa wingi katika mchezo wetu ujao wa ligi dhidi ya Namungo, kwani wachezaji wameahidi kuipambania timu kupata matokeo mazuri.

“Wachezaji wamenipa ahadi hiyo ya ushindi, baada ya kufanya nao kikao kizito kabla ya kuanza mazoezi jana (juzi) uwanjani, hivyo watarajie makubwa baada ya kuwataka kusahau matokeo yaliyopita,” alisema Cadena.

Nahodha wa timu hiyo, John Bocco, alisema: “Kama wachezaji tumefanya maandalizi mazuri kulingana na mpinzani tunayekwenda kukutana naye, tumesahau matokeo yaliyopita, hivyo tunajiandaa na mchezo ujao dhidi ya Namungo.”

STORI NA WILBERT MOLANDI

Leave a Comment