ILIPOISHIA RISASI JUMAMOSI:
“Humo ndani hakuna mtu wenyewe wamekwenda kazini na leo watachelewa kurudi,” yule afande aliyetaka penzi kwangu muda mfupi uliopita alimfahamisha mwanamke huyo.SHUKA NAYO…
Mimi nilibaini ni mama haraka sana, nikashtuka!
“Nimekuja kumfuata mwanangu, yupo humu ndani?” mama alimuuliza yule afande.
“Yule binti mzuri, mfupi hajasuka nywele?” yule afande ambaye hakumfahamu mama alimuuliza. Mimi moyoni nikawa nasema we afande, mbona unajiweka kimbelembele sana, una nini lakini?
“Ndiyo huyohuyo!” mama alijibu.
“Yupo ndani na dakika chache nilikuwa nazungumza naye, wewe ingia hapo ndani kisha bisha hodi kwenye mlango wa kulia kwako,” yule afande alimwambia mama.
Kila kitu kikawa wazi sasa.
Wakati mama Rhoda anatembea kuelekea alikoelekezwa, yule afande akamwomba samahani, aliposimama akamwuliza kama ni kweli mimi nilikuwa mwanaye wa damu.
“Ni binti yangu kabisa, leo nimemfuata nataka arudi nyumbani. Binti ni malaya sana huyu, ananitia aibu kubwa. Mimi mama yake sikuwahi kuwa hivi,” mama alifoka.
“Kwa hiyo mama unataka kuondoka naye au?” aliuliza afande.
“Si mwanangu,” alisema mama kwa sauti ya kuwaka akimaanisha swali la afande lilikuwa la hovyo.“Da! Mimi nilizungumza naye kitu fulani mama. Sasa kama unaondoka naye, basi ungeniacha nimalize naye mazungumzo,” alisema yule afande mpaka mimi nikahisi hana akili nzuri kichwani…
“Yanahusu nini?” mama alimuuliza akiwa anagonga mlango wa chumba nilichokuwemo…
“We malaya,” mama aliniita kwa jina hilo.
Niliumia sana moyoni. Mama yangu mzazi kuniita mimi malaya.
“Abee,” niliitika kwa nidhamu ya hali ya juu.
Nilikwenda kufungua mlango huku moyoni nikiwa namlaani sana yule afande kwa kumwambia mama kwamba nilikuwemo ndani.
Nilipofungua tu mlango, nilikutana na uso wa mama. Alinishika mkono na kunitoa kwa nguvu kwenye chumba hicho…
“Leo ndiyo utajua mimi ni nani?” alisema.
Nilimsihi mama aniache nizirudie sendozi zangu lakini alikataa, nikawa natembea pekupeku.
Yule afande alitoa kichwa chumbani kwake kutuangalia. Akatingisha kichwa…
“Mama ungemwacha afunge basi japo mlango wa watu,” alisema yule afande…
“Kwani na nyie mnaibiwaga!?”
Sasa kazi ilikuwa ni kuikata mitaa, kutoka upande wa Hospitali ya Temeke, kuvuka barabara na kuingia upande wa pili kuelekea Mtaa wa Wailes ambako ndiko nyumbani.
Mama kama kawaida yake, wakati akinikokota, mimi nilikuwa kwa nyuma, yeye mbele ila mkono wangu wa kulia ndiyo ulikuwa mkononi mwake. Vuta picha hapo nilikuaje?!
Watu njiani walikuwa wakinicheka, wengine walinijua wakasema…
“Rhoda leo vipi! Polisi nini? Pole wa kwetu.”
Sikuwa na muda wa kuwajibu si kwa kupuuza bali kwa kasi ya kupelekeshwa.
Sikujua ni kwa nini kama mama alishindwa kujua kwamba aibu ninayoipata hata yeye inamhusu. Maana kama mimi ni malaya, yeye anahusika kwa sababu si ndiyo mlezi wangu!
Kufika mtaani sasa, ndiyo usiseme. Wasichana wenzangu walitoka majumbani kwa kuitana kiumbeya…
“Jamani Rhoda kakamatwa na mama yake, alilala kwa mwanaume,” alisema binti mmoja anaitwa Pashuu.
Mama aliniingiza ndani, chumbani kwangu, akaniweka kitandani…
“Vua nguo nakwambia,” alisema kwa ukali mama.
Moyoni nilishangaa sana mama kuniambia nivue nguo kwani nilijua anajua mimi nilikuwa kwa mwanaume maana aliniacha mwenyewe, japo ni kwa wanaume, sasa alitaka nivue nguo ili iweje?
“Sasa mama nikivua nguo halafu…”
“Weee! Paka shume we,” mama alikuja juu.
Ilibidi nivue ili nisubiri hatua nyingine kutoka kwake. Nilipomaliza nikabaki nimemtumbulia macho kumwangalia tu…
“Enhe! Ulilala naye?”
“Nani mama?”
“Pumba** kwani nilikuacha kwa nani?” mama aliniuliza huku akinipiga…
“Ndiyo mama.”
“Yupi?”
“Mhh!” Swali hilo la mama lilinifanya nigune kwanza. Yupi kivipi wakati anajua aliniacha kwa nani!
“Sijakuelewa mama.”
“Hujanielewa nini? Wewe si ulikuwa chumba cha kushoto? Mbona leo umetokea chumba cha kulia?”
Moyo ulifanya paa! Nikaamini kwamba, kweli mzazi ni mzazi tu, huwezi kumdanganya! Kumbe mama alijua niliingia chumba cha kushoto na amenikuta chumba cha kulia…
“Alihamia kule.”
“Wewe, siyo kwamba umewachanganya? Nakujua mwanangu Rhoda.”
“Hapana mama alihamia kule. Lakini ni yuleyule.”
Mama aliniacha, akaniambia ni marufuku kuanzia siku hiyo kutoka hata kufika kibaraza cha nyumbani. Akasema nikija kuvunja amri yake hiyo nitakiona cha moto!
***
Saa tisa usiku siku hiyo, nikiwa chumbani kwangu nimelala, simu yangu iliita, kuangalia hivi ni afande Mwita anapiga, sikupokea.
Alipiga kama mara saba, alipoacha ikaingia simu ya afande Chacha, nayo iliita weee, sikupokea. Ikaja simu ya afande Mwira, nayo ikaitaa weee sikupokea! Nikaanza kuogopa sasa.
“We Rhoda, hiyo simu inatoka wapi usiku huu?” mama aliniuliza kutokea chumbani kwake…
“Siijui namba mama, labda amekosea.”
Nilichofanya, niliamua kuizima simu. Lakini kabla sijafanya hivyo, meseji iliingia. Ilitoka kwa afande Chacha, yaani yule wa kwanza kabisa mbaba, aliandika…
“Utakula jeuri yako.”
“Poa,” nilimjibu, ndiyo nikazima simu.
Nilipata tabu kuupata usingizi maana muda mwingi nilikuwa najifikiria ni kwa nini walinipigia simu wote? Ina maana wako pamoja? Kivipi?
***
Mwezi mmoja ulikatika bila kupata mawasiliano kutoka kwa yeyote kati yao. Lakini siku hiyo niliamka ninaumwa. Afya haikuwa njema. Nilipokuwa najisaidia, nilisikia maumivu makali sana, halafu sehemu ya chini ya tumbo ikawa inauma pia…
“Mama,” nilimwita…
Je, unajua nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi ili kujua zaidi ya leo.
Gono hilo!