×

ALIYEUAWA NA POLISI FAMILIA YALIPWA MAMILIONI

MARA: Mkuu wa Kitengo cha Haki za Binadamu katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Robert Farrar uliopo mji mdogo wa Nyamongo, Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara amejutia kuuawa kwa risasi marehemu Mgosi Magasi Chacha na askari Polisi wanaolinda mgodi huo kwa kuwalipa wazazi wa marehemu mamilioni ya shilingi kama kifuta machozi.

Chacha alipigwa risasi mgongoni na kisha kutokea tumboni na askari polisi mwaka 2012 alipokuwa katika eneo la mgodi huo akiokota mawe ya dhahabu na kuwaacha wazazi wake Samwel na Mariam Magasi Chacha wakiwa na hali mbaya kiuchumi kwa kuwa walikuwa wakimtegemea yeye kwa kila kitu kutokana na umri wao kuwa mkubwa.

Farrar baada ya kufika nyumbani kwa wazazi wa Chacha alisema kuwa anaomba radhi familia kwa kupoteza mtoto wao waliyemtegemea kuwatunza katika umri wa uzee wao na familia yake aliyoiacha ya mjane Elizabethy Mgosi Magasi na watoto wake watatu waliobakia yatima hadi sasa.

Mkuu huyo alisema kuwa endapo angelikuwa katika kitengo hicho enzi hizo, angelikomesha mauaji ya kiholela yaliyokuwa yakitokea kwa wananchi waliowahi kuuawa na askari Polisi na walinzi wa mgodi huo waliofahamika kuwa ni Mobiles.

Alisema kwa mujibu wa haki za binadamu na sheria, haziruhusu mtu kuuawa badala yake sheria zinasema anapaswa kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria wanapovunja sheria kama ilivyotokea kwa marehemu Chacha.

“Kufuatia matukio ya vifo vilivyotokea marehemu kupoteza uhai wao, ndugu, wazazi, na familia zao walibakia kuathirika kisaikolojia na kupata madhara ya kiuchumi kwani waliomtegemea kwa mahitaji mbalimbali alikuwa hayupo hivyo kukosa huduma mbalimbali,” alisema.

Chacha aliuawa akiwa na umri wa miaka 23 na Farrar alionesha kuguswa na wazazi wa marehemu huyo kusema kuwa anaamini hadi sasa wazazi hao hajamsahau kijana wao licha ya watu wengine kusahau tukio hilo.

Farrar hivi karibuni aliwakabidhi wazazi wa marehemu huyo Samwel na Mariam Magasi Chacha hundi mbili za fedha jumla ya shilingi milioni 21,000,600 za Kitanzania zilizogawanywa katika hundi mbili moja ikiwa ya shilingi milioni 5,200,000 na nyingine ya shilingi milioni 15,900,600 na shughuli hiyo ilifanyika katika Hoteli ya Gold Land iliyopo mjini Tarime na aliambatana na maafisa wake wa uhusiano wa mgodi huo.

Fedha hizo alidai zinatolewa ili kukarabati nyumba ya wazazi wa marehemu huyo na zingine za kujikimu na za kununua ng’ombe wa maziwa na kulimia, ikiwa ni sehemu tu ya fidia ya madhara ya kiuchumi waliyoyapata kutokana na kifo cha marehemu aliyekuwa akiishi na kuzalisha mazao, na uendeshaji wa bodaboda na shughuli zingine halali enzi ya uhai wake.

Mjane wa marehemu, Elizabeth Mgosi Magasi aliwahi kupatiwa shilingi milioni 26 kama mirathi kutokana na kufiwa na marehemu mumewe ili zimsaidia kutunza familia yake ya watoto watatu alioachiwa na mumewe.

‘’Mimi nilipatiwa fedha hizo na mgodi huo baada ya kuhangaika sana nikisaidiwa na shemeji yangu mkubwa, Roberty Marwa tulipoungana na kufuatilia haki zetu,” alisema mjane huyo. Alisema walipatiwa bima ya afya na wazazi kuahidiwa na Farrar kupatiwa bima ya afya itakayodumu kwa muda wa miaka mitano na kwamba baada ya kumalizika muda wake huo mgodi huo utawaongezea tena muda wake.

STORI  IGENGA MTATIRO, UWAZI