
HAMASA kuelekea kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga SC dhidi ya Al-Ahly ya Misri, imeanza kwa nguvu baada ya Yanga, kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 40.
Yanga imefungua kampeni zao visiwani Zanzibar, jana Jumatatu, huku ikiingia udhamini wa siku saba wenye jumla ya shilingi milioni 40 kutoka Zanzibar Revenue Authority (ZRA) na Zanzibar Investment Promotion Authority (ZIPA) ambapo kila moja imetoa shilingi milioni 20.

Mbali na hivyo, mchezo huo wa Kundi D utakaochezwa wikiendi hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, umepewa jina la Bacca Day.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, amesema: “Bacca Day inanogeshwa zaidi na udhamini tulioupata kwa ajili ya mchezo huu utakaofanyika Desemba 2, Yanga SC tumepata milioni 20 kutoka ZIPA na milioni 20 kutoka ZRA, ambazo jumla ni milioni 40.
“Ibrahim Bacca ni mchezaji wetu kutoka hapa visiwani. Leo tupo hapa kwa ajili ya kuzindua Bacca Day na kilele chake kitafanyika Desemba 2, Benjamin Mkapa.”