
SERIKALI ya Tanzania, imesema haitumii nguvu katika kuwaondoa wananchi jamii ya kimasai wanaoishi Hifadhi ya Ngorongoro, bali inawaondoa kwa hiari ili kuilinda hifadhi hiyo.
Hayo yamebainishwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, Disemba 15 2023, ikiwa ni siku moja tangu Bunge la Umoja wa Ulaya (EU), ishauri uchunguzi huru ufanyike ili kuangalia namna ya kushughulikia sakata hilo pasina uvunjifu wa haki za binadamu.
“Serikali inaendelea kusisitiza kwamba, zoezi hili ni la hiari. Wananchi waepukane na taarifa potofu kuwa kuna uvunjwaji wa haki za binadamu au uondoaji wa watu kwa kutumia nguvu. Moja ya sababu za kuwahamisha ni usalama wa wananchi na kulinda eneo la Ngorongoro ili libaki salama,” amesema Matinyi.
Matinyi amesema Serikali iliamua kuchukua uamuzi wa kuwaondoa kwa hiari wananchi, ili kudhibiti ongezeko la idadi ya watu na mifugo, inayodaiwa kuhatarisha uwepo wa hifadhi hiyo.
Alisema idadi ya watu imeongezeka kutoka 8,000 waliokuwa wanakaa asilimia 37 ya sehemu hiyo yenye ukubwa wa ekari 8,292, hadi kufikia watu 115,000 na mifugo 800,000.
Kuhusu zoezi la kuwaondoa wananchi, Matinyi alisema Serikali imetenga maeneo maalum kwa ajili ya wanaotaka kuhamia kwa hiari, ambapo wanahamishwa bure pamoja na kulipwa fidia.
Amesema maeneo hayo yamejengwa miundombinu ya ufugaji, pamoja na huduma nyingine za kijamii.
Jana tarehe 14 Disemba 2023, bunge la EU lilipitisha azimio la kuiomba Serikali ya Tanzania, kuruhusu waangalizi wa EU kutembelea katika maeneo yenye mgogoro.