
BAADA ya kusimama kwa zaidi ya miezi mitatu, hatimaye uhondo wa Ligi Kuu Bara umerejea.
Mabingwa wa msimu uliopita, Yanga, watakuwa wakipambana kulitwaa taji hili mara ya nne mfululizo, wakati timu nyingi zinaonekana kufanya usajili mzuri ambao ulithibitishwa na mechi za wikiendi iliyopita, kwa jinsi zilivyokuwa na msisimko mkubwa.
Championi Jumatatu linakuletea timu ambazo zinaonekana zitasumbua vikali msimu huu na kuchuana katika nafasi za juu.

AZAM FC
Wengi wanawadharau kwa kuwa hawajafanya usajili wa kutisha. Lakini niionavyo Azam, naamini itawaumbua wengi. Imeondokewa na wachezaji nyota kadhaa wakiwemo Erasto Nyoni, Aishi Manula na John Bocco waliotua Simba pamoja na Gadiel Michael aliyetua Yanga lakini bado ina vijana wengi wenye vipaji pamoja na wakongwe.
Imefanya maandalizi mazuri. Ukiangalia mechi zake za kirafiki, imeshinda nyingi, na ndiyo timu iliyocheza mechi nyingi zaidi za kimataifa za kirafiki kuliko nyingine.
Mechi za kirafiki walizocheza Rwanda na baadaye Uganda, zitakuwa zimewapa somo kubwa. Mechi nyingi za kirafiki, zimemfanya kocha Aristica Cioaba kutambua kikosi chake cha kwanza tofauti na wapinzani wake wengi, pia hata wachezaji wenyewe wametambuana vizuri.

MBEYA CITY
Itakumbukwa msimu uliopita ilipozikazia timu kubwa za Simba na Yanga. Ingawa makali yake yamepungua tofauti na ilivyopanda ligi kuu miaka kadhaa iliyopita na kushika nafasi ya tatu, bado naiona ni timu sumbufu, licha ya kuondokewa pia na wachezaji wake kadhaa muhimu.
Ina wachezaji kadhaa wenye uzoefu wakiwemo Mrisho Ngassa, Haruna Shamte na Hassan Mwasapili.
Bado ina mgogoro na kocha wake Mzambia, Kinnah Phiri lakini natarajia kuiona ikichuana katika nafasi za juu.

SINGIDA UNITED
Japo imepanda daraja msimu huu lakini kwa usajili ilioufanya pamoja na udhamini mkubwa ilionao wa kampuni ya kubashiri matokeo ya SportPesa, naiona ikiwa haimuachi mtu salama.
Nguvu nyingine kubwa iliyonayo ni kocha mzoefu Hans van Der Pluijm aliyewahi kuinoa Yanga. Lakini kikubwa imefanya usajili wa kutisha kuliko timu nyingine zote ndogo na imefanya maandalizi mazuri.

YANGA
Awali wengi wa lionekana kuibeza Yanga kutokana na kuamini msimu huu haijasajili vizuri, hasa baada ya kuondoka kwa Haruna Niyonzima na Simon Msuva, lakini iliwaumbua wengi Juma tano iliyopita katika mchezo wa Ngao ya Jamii pale ilipoipelekesha Simba licha ya kufungwa kwa penalti.
Yanga kwa asilimia kubwa ni kikosi kilekile kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo, lakini imejiboresha sana kwa kumsajili Mcongo, Papy Kabamba Tshishimbi na Ibrahim Ajibu kutoka Simba. Kwa hiyo, imekuwa safu pana na imara ya ushambuliaji ikiwa pia na masupastaa Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Obrey Chirwa.
Kombinesheni ya Tshishimbi, Thaban Kamusoko na kiungo mwingine mpya Rafael Daudi, inaonekana itasumbua vilivyo kwenye ligi, hasa katika kiungo.
Baadhi ya mashabiki wanadhani Yanga hii ni dhaifu sana, wakiilinganisha na Simba kwa usajili waliofanya lakini nikwambie tu kuwa kwa mtazamo wangu, hakuna timu itakayokuja kufanya vyema kama Yanga, kwani Simba wamesajili wachezaji bila ya kuangalia wapi kulitakiwa kuzibwa gepu. Tatizo pekee linaloweza kuwaondoa relini labda ni ukata, kwa kuwa inaonekana hawana vyanzo vya uhakika vya mapato.
SIMBA SC
Hawa jamaa safari hii wametisha kutokana na kuwa na kikosi kipana na chenye majina makubwa ya wachezaji, lakini siku zote kujiamini kwingi kuna madhara makubwa.
“Mpira ni tofauti na draft, ukikutana na anayejua basi jua utapigwa supa lakini tofauti na mpira wa miguu unaweza ukawa unajua lakini ukafungwa,” kauli hii aliitoa msemaji wa Simba, Haji Manara, kikosi chao cha bil 1.3 kimekuwa tishio kubwa msimu huu kwani kimeanza vyema maandalizi yake.
Kwa usajili waliofanya na jinsi timu hiyo ilivyo na hamu ya kuchukua ubingwa wa ligi kuu msimu huu moto watakaouwasha siyo wa kitoto.
Sasa ina wachezaji wengi wazoefu, mfano Emmanuel Okwi, John Bocco, Niyonzima, Shiza Kichuya, Aishi Manula, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe pamoja na wenye vipaji kama Mohammed Ibrahim, Mzamiru Yassin na wengine. Wanahitaji kuzoeana tu waanze kufanya yao.
KAGERA
Timu hii ipo kimya lakini moto wake ni kama wa kifuu, huwa unawakia ndani kwa ndani. Msimu uliopita walimaliza nafasi ya tatu na kocha wao Mecky Maxime akachukuwa tuzo ya kocha bora.
Msimu uliopita walimaliza nafasi ya tatu chini ya Simba na Yanga, ukiachana na usajili wao mdogo waliofanya lakini kocha wao Maxime ndiyo mpango mzima. Mara zote hutoa ushindani mkubwa, tangu alipokuwa Mtibwa.
Ibrahim Mressy, Dar es Salaam