ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Sasa nyumba yote ikawa ni maombi tu. Kukemea kwa sana hali iliyonizidishia maumivu makali sana ya kuchomwa moto mwilini. Nilianza kujinyonganyonga kuashiria kwamba, maumivu ya moto niliyasikia kwa undani zaidi kuliko awali.
Nikawaona wale jamaa zangu nao wamejitokeza. Sasa ikawa wamejitokeza laivu!!
SASA ENDELEA…
Lakini kwa maombi mazito ya mchungaji, wakapotea ghafla, kukawa kimya. Nilikaa kitandani nikiwa natweta kwa wasiwasi na hofu kuu!
Cha kushangaza, mchungaji palepale akawaambia wenzake waondoke kwenda kanisani. Alikuwa akitokwa na jasho jingi sana na mimi ninavyofahamu, mtu akiomba sana hasa pale anapopambana na pepo wachafu, jasho lazima.
Hapa niseme kidogo. wengi wanadhani kusali ni jambo la kawaida. Si kweli. Kusali ni mapambano tena mapambano makubwa sana. Mtu anaposali, pembeni yake au mbele yake kunakuwa na pepo wachafu ambao wanamrushia ‘mishale’ ili anayeomba achoke.
Mfano, umewahi kusali huku umefumbua macho. Kinachotokea ni kwamba, pepo
chafu anakufuata na kukuingia kimawazo. Si kimwili, kimawazo. Matokeo yake sasa, ukiona fagio chini huku unasali unawaza; ‘hili fagio karibu linaisha, itabidi ninunue jingine.’ Ukiona kapeti chini unawaza; ‘kapeti langu limechakaa sana, si sawasawa na lile la kwa mama Anna, lake jipya.’
Au utakuta mtu anaomba amesimama, akifumbua macho kuangalia ukuta, anajiwa na mawazo; ‘huu ukuta sasa ubadilishwe rangi, iwe ya bluu ya bahari. Rangi hii imepauka sana lakini nayo imekaa tangu mwaka juzi.’
Kwa mawazo haya, huwezi kusali sawasawa. Na mawazo hayo yote huwajia watu wanapokuwa kwenye maombi kwa lengo la kuvuruga mtiririko wa sala.
Basi, wote waliondoka, akabaki mke wangu tu. Tukawa tunatazamana bila kusema lolote. Mwili wangu ulikuwa umelegea kwa kuchoka huku nikiwa nawaza kupanda kitandani kulala.
“Hivi mume wangu kwani unanificha nini mimi?” mke wangu aliniuliza.
“Kwani nakuficha nini?”
“Wewe una mkataba na majini?”
“Sema sina mkataba wa majini,” mwanamke mmoja, mweupe alisimama ukutani ghafla na kuniambia maneno hayo.
“Sina mkataba na majini,” nilisema.
“Sasa ni kwa nini walikuja kukupigania kama huna mkataba nao?”
“Muulize walikuja kukupigania saa ngapi?” yule mwanamke alinielekeza.
“Walikuja kunipigania saa ngapi na wapi?” nilimjibu na kuongezea langu la na wapi.
Mke wangu hakunijibu, aliendelea kuniangalia kwa muda kisha akatingisha kichwa. Mimi nikamwangalia yule mwanamke, akaachia tabasamu na kusema:
“Mapambano ni makali sana, mkeo ameamua kutumaliza lakini sisi tumeweka kikao kwa ajili yake na kuamua kumuua mapema ili asije akaleta madhara.
“Tumekuwa tukimvumilia sana kwa ajili yako lakini sasa imefikia tamati. Lazima mkeo afe ili wewe ufanye kazi kwa usahihi mkubwa na kunufaika. Suala la namna gani utaishi tunajua sisi.
“Njia tutakayoitumia kumuua mke wako ni kwa kumkaba koo mara moja na kuvunja mishipa ya shingoni. Ili tumpe maumivu makali tunasubiri akiwa amekwenda kuchota maji. Atavunjwa shingo akiwa na ndoo kichwani.
“Kuhusu suala la msiba, mkeo akishafariki dunia hutatakiwa kulia ili kulinda uhai wako. Hutakiwi kuweka wazi huu mkakati. Hutakiwi kuweka matanga kwa siku kadhaa hapa nyumbani kwako. Ukishazika, weka wazi msimamo wako kwamba hakutakuwa na matanga na msiba utakuwa umekwisha.”
Alipomaliza maelezo au maagizo hayo, yule mwanamke alipotea ghafla mbele ya macho yangu! Nilifikicha macho ili kuangalia vizuri.
“Lakini kama hutaki kuniambia kilicho kwenye siri yako sawa,” alisema mke wangu. Akapanda kitandani kulala na mimi nikapanda kitandani kulala.
Nilikosa usingizi. Muda mwingi nilikuwa namfikiria mke wangu, eti kwamba majini watamuua. Tena watamuua kwa kumkaba koo na kisha kumvunja mishipa ya shingo. Na eti watamvizia akiwa ana ndoo ya maji kichwani ili kumuongezea maumivu! Iliniuma sana. Yale maneno ya yule jini mwanamke yalijirudia kichwani mwangu…
“Njia tutakayoitumia kumuua mke wako ni kwa kumkaba koo mara moja na kuvunja mishipa ya shingoni. Ili tumpe maumivu makali tunasubiri akiwa amekwenda kuchota maji. Atavunjwa shingo akiwa na ndoo kichwani.
“Kuhusu suala la msiba, mkeo akishafariki dunia hutatakiwa kulia ili kulinda uhai wako. Hutakiwi kuweka wazi huu mkakati…”
***
Kulikucha kwa tabutabu, mke wangu akatangulia kutoka kitandani huku akisema anakwenda kuchota maji. Niliogopa sana. Nilipotaka kumwambia asiende yule jini mwanamke akatokea ghafla.
“Hutakiwi kuweka wazi huu mkakati. Zingatia hilo kwa ajili ya usalama wa uhai wako. Hii ni amri, wala si maoni yetu,” alisema na kufutika.
Nilibaki namwangalia mke wangu, naye akasema:
“Kuanzia leo nimeamua kufunga na kuomba. Itakuwa kwa muda wa siku tatu.”
Je, wewe msomaji unajua kilichotokea? Usikose kusoma wiki ijayo kwenye gazeti hili.