
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika mwaka wa masomo 2023/2024 Serikali imetenga Sh. bilioni 48 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya stashahada.
Amesema hayo Jumanne, Januari 16, 2024 wakati wa ufunguzi wa Chuo Kikuu Katoliki Mbeya (CUoM) mkoani Mbeya.
Amesema kuwa mpango huo ambao ni maono na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unalenga kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na kuwezesha wahitimu wa vyuo nchini kujiamini na kumudu ushindani wa kitaifa na kimataifa.
“Lengo jingine la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ni kuona vijana wengi wanapata elimu itakayowapa ujuzi na uwezo wa kushiriki katika ujenzi wa Taifa”.