×

Hoja Ya Mbunge Shabiby Tozo Za Simu Kupiga Tafu Mfuko Wa NHIF, Ilivyopokelewa

Mbunge wa Jimbo la Gairo mkoani Morogoro, Ahmed Shabiby.

Siku mbili baada ya Mbunge wa Jimbo la Gairo mkoani Morogoro, Ahmed Shabiby kuishauri serikali kuweka sh 2,000 katika tozo za huduma za simu za kila mwezi ili makusanyo yake yaende kwenye Mfuko wa Taifa wa Afya ya Bima ambao unasuasua, raia nao wameijadili hoja yake hiyo.

Wakizungumza na mwanahabari wetu kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema hoja ya mbunge huyo siyo mbaya kama itasimamiwa vizuri.

Saimon Masawe, mfanyabiashara wa mitumba Soko la Karume, Ilala jijini Dar, yeye alisema kuwa, NHIF imekuwa ikisuasua kila wakati kutokana na uhaba wa fedha.  Hivyo akaitaka serikali ichukue ushauri wa mbunge huyo.

“Utaratibu wa Bima ya Afya kwa wote ni sawa kwa sababu siku hizi magonjwa ni mengi sana. Lakini tatizo ni kipato cha baadhi ya wananchi hakiwezi kuwafanya wakakata bima ya afya kama serikali inavyofikiria.

“Hivi unajua kuwa, kuna Watanzania hawashiki shilingi elfu ishirini hata miezi sita?! Hawa watakata Bima ya Afya kweli?” Alihoji Saimon.

Naye Aisha Zuber, mkazi wa Sinza A yeye alisema kuwa, aliifuatilia hotuba ya mheshimiwa Shabiby kwa umakini.

“Mimi kipindi cha bunge nakifuatilia sana. Shabiby alichosema ni ili kuunusuru Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Ana hoja. Juzi kati tu kuna baadhi ya watoa huduma walitangaza kujitoa. Ni kwa sababu ya matatizo ya pesa.

“Kwa hiyo mheshimiwa Shabiby aliposema anaiomba serikali iweke shilingi 2,000 kwa ajili ya mfuko wa Bima ya Afya uweze kujiendesha lengo lake ni kuwatetea wanyonge lakini pia kuisaidia serikali jinsi ya kuondokana na changamoto za watoa huduma kujitoatoa,” alisema Aisha.

Fred Camilius ambaye ni mkazi wa Mbezi Mwisho, Dar. Alisema serikali kama itakuwa makini itabidi ichukue hoja ya mbunge huyo kwa sababu imelenga kumsaidia mwananchi mnyonge.

“Wakati nasikia unakuja mpango wa bima ya afya kwa wote na kwamba kila familia itatakiwa kulipiwa. Nilikuwa na wasiwasi wa uwezo wa Watanzania wenzangu.

“Ukitaka kujua itakuwa shida kila mwananchi kukata bima ya afya angalia watu tunavyowasiliana. Utakuta ndugu zetu hasa vijijini, kila siku anakubip, ukimpigia anakuomba vocha. Ukiangalia vocha zipo hata za shilingi mia tano. Lakini watu hawana pesa. Huo mfuko wa bima ya afya itabidi serikali ifuate ushauri wa watu kama hawa ili uweze kujiendesha,” alisema Fred.

Akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2024/2025, mheshimiwa Shabiby aliiomba serikali kuweka tozo ya Shilingi 2,000 kwa mwezi katika mitandao ya simu sambamba na mazao ili kuisaidia NHIF kuendelea kujiendesha na kuwahudumia wananchi ipasavyo.

Mheshimiwa Shabiby alisema hatua hiyo itakuwa mkombozi kwa mfuko huo ili kuondoa malalamiko ya mara kwa mara.

“Kwa hili wanaweza kulikubali au wasilikubali wengine watatukana kwenye mitandao ya kijamii, lakini acha watukane maana kuna watu hawapo duniani na hata mbinguni hawako. Lakini siwezi kuogopa kwa sababu mtu atatukana.

“Ili kuinusuru Bima ya Afya. Kuna umuhimu wa kuwapo chanzo ambacho kitakuwa cha uhakika katika kuchangia mfuko huo kwani wananchi wameshindwa kuchangia Shilingi 30,000 kwa ajili ya Bima ya CHF na hivi hatujajua hiyo bima kwa wote itakuwa na kiwango kipi,” alisema.

Shabiby alisema ikipangwa Shilingi 300,000 na Sh.60,000 kwa matibabu ya kawaida wananchi wa vijijini kuimudu itakuwa vigumu, hivyo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kama inavyohitajika, hivyo ni wakati wa wananchi kujionea huruma ili kuokoa mfuko huo.

“Ukiangalia katika mipango ni kutaka kuwachangisha wananchi lakini namna ya kupata hii fedha itakuwa vigumu kama ilivyokuwa kwa CHF na leo hii ukiangalia wanufaika wa bima katika watanzania 100 ni watu wanane tu ambao wanalipa.

“Hii inaonesha hatuna chanzo maalum cha kuchangia mfuko huu, kwakusaidia watu wasiyokuwa na uwezo wapate matibabu,”alisema.

Alitaja njia za kupata chanzo hicho cha uhakika kuwa ni pamoja na kuweka tozo katika mitandao ya simu ambayo inatumiwa sana nchini.

Alisema kuna laini zaidi ya milioni 72. Alisema ikiwekwa tozo ya Shilingi 2,000 kwa mwezi kwa mwaka itakuwa Sh. 24,000 sawa na Shilingi trilioni 1.728 kwa idadi ya laini hizo.

Mbunge huyo alishauri pia watumiaji wa mitandao hiyo wenye hadhi kama vile wabunge, wafanyabiashara, wafanyakazi kiwango kiongezwe hadi Sh.10,000 au 15,000 na kuunganishwa na kupatikana zaidi ya Shilingi trilioni mbili.

“Pamoja na kuwapo kwa kiwango hicho, wananchi wa vijijini wasiwekewe ukomo wa matibabu kutokana na kuwa na kipato kidogo ambapo wamekuwa wakikosa matibabu na dawa za muhimu,” alisema.

Shabiby alisema viwango vingine vitafutwe hata kwenye mazao ambako kila kilogramu moja itatozwa Sh. moja au mbili kwa kuwa hata mkulima atanufaika na bima hiyo.

“Sasa kwa wale ambao hawana simu, hiyo inadhihilisha kuwa ni maskini wa kutupwa, hivyo hata hicho kiasi kidogo wasitozwe, atatibiwa kutokana na vyanzo hivyo vya mifuko,” alisisitiza.

Aidha, mheshimiwa Shabiby alishauri zahanati za vijiji pamoja vituo vya afya vibinafsishwe kwa watu akitolea mfano, nchi ya Korea Kusini ambako wamefanya hivyo kwa kuwekwa kwenye mfumo mmoja, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utolewaji wa huduma za afya.

Alisema kuwapo kwa mfumo huo wa ufuatiliaji wa vituo vyote vya kutoa huduma za afya, utasaidia kudhibiti vitendo vya udanganyifu katika mfuko wa bima ikiwa ni pamoja na kusaidia ongezeko la wahudumu wa afya.

Leave a Comment