
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa mwaliko rasmi kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Uturuki kushiriki Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayotarajiwa kufanyika nchini mwishoni mwa mwezi Juni 2024.
Rais Dkt. Samia ametoa mwaliko huo wakati akifungua rasmi Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki lililofanyika Aprili 19, 2024 jijini Istanbul na kuhudhuriwa na zaidi ya wafanyabiashara na wakezaji 200 kutoka nchi hizi mbili.

Amesema maonesho hayo ya biashara ambayo ni makubwa Afrika Mashariki hutoa fursa ya kuwakutanisha wafanyabiashara na kuwawezesha kubadilishana taarifa na uzoefu, kujua taarifa mpya za masoko na bidhaa pamoja na kuuza bidhaa.
Kadhalika Rais Samia ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uturuki kuja kuwekeza nchini na kuitaja Tanzania kama nchi yenye fursa lukuki kama vile ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, Hifadhi za wanyama kwa ajili ya utalii, nishati, madini ikiwemo Tanzanite ambayo hupatikana nchini Tanzania pekee na fursa na biashara na uwekezaji.
Amesema Serikali yake imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji ambapo pamoja na mambo mengine imewekeza katika kujenga miundombinu inayoiunganisha Tanzania na nchi nyingine jirani ikiwemo Reli ya Kisasa ya SGR.