Nilimwangalia bosi wangu wa kike kwa jicho la kumshangaa kwa maneno yake makali kwangu huku akijua mimi siwezi kumzunguka kwa mume wake lakini naye akazidi kukazania anachokiamini…
“Tena nikwambie kitu we dada, mimi hapa si mjinga. Nina akili zangu timamu na najua nini ni nini! Acha kabisa tabia ya kuvaa vizuri hapa nyumbani kwangu. Nakulipa mshahara, badala ya kumtumia mama yako kijijini, wewe unanunua pafyumu,” alinisema bosi wangu mama Rehema…
“Lakini mama ina maana nikitaka kununua kitu ninachokipenda niache wakati pesa ninayo?”
“Jamila nakuheshimu sana…tena narudia kusema nakuheshimu sana Jamila. Kwanza unavaa vizuri ili umzidi nani humu ndani. Wewe unaweza kunizidi mimi wakati bado unanuka maziwa!” bosi wangu alinichamba ile mbaya.
Niliamua kuondoka kwenda chumbani kwangu, nikafikia kwenye kitanda na kujitupa nikimuwaza bosi wangu mama Rehema…
“Dada nataka juisi,” Rehema aliingia chumbani na kuniambia hivyo.
Nilitoka chumbani huku nikitamani kumsukumia mbali Rehema ili kumkomoa mama yake…
“Hamjambo hapa?” baba mwenye mji sasa alisalimia kwa sauti nzito ya kiume…
“Hatujambo, za kazi mume wangu?” mama Rehema alianza kusalimia…
“Shikamoo baba…” huyo alikuwa Rehema…
“Shikamoo baba,” mimi nilisalimia huku nikimpokea magazeti…
“Wewe Jamila nenda jikoni, kwani magazeti Rehema hawezi kupokea?”
“Mh!” Niliguna na kwenda zangu jikoni.
Nyuma yangu wakati nakwenda jikoni nilimsikia baba Rehema naye akishangaa na kumuuliza mkewe kisa cha kunizuia nisipokee magazeti…
“Kwani Rehema ana nini?” mama Rehama alijibu kwa mkato…
“Kama hana kitu kwa nini hakunipokea wakati naingia na alisimama mlangoni?” baba naye alizidi kutetea…
“Baba Rehema, mbona kama unamtetea sana huyu msichana wa kazi! Kuna nini kwani kati yenu?” eti mama alinishuku, nikamshangaa sana. Mimi na mume wake tunaweza kuwa na nini kwani!
Nilianza kujifikiria upya nikiamini kwamba, ndani ya nyumba ile sitadumu. Hapo ndiyo kwanza nilikuwa na siku kumi na saba tu.
Usiku uliingia, mama Rehema alisema anajisikia kichwa kinauma, akanituma dawa dukani. Nilisema hiyo ndiyo nafasi yangu ya kutimua moja kwa moja maana alinipa noti ya shilingi elfu tano. Nilisema nibebe begi langu, nikapande daladala nirudi kwa wakala mtu aliyenitafutia kazi kwa mama Rehema.
Niliingia chumbani, mama Rehema aliponipa pesa akaenda chumbani. Sebuleni alibaki baba tu. Rehema naye alikuwa chumbani kwake.
Nikiwa nimeshabeba begi, nilitoka kusoma mazingira. Nikakutana na baba Rehema akienda chooni…
“Jamila,” aliniita, nikaogopa sana, nikaitika kwa sauti ya chini ili mama asisikie kule chumbani…
“Inabidi umzoee mama Rehema. Mama Rehema huwa hamwamini mtu. Sasa angalia, hapa nyumbani si amekuleta yeye?”
“Ndiyo baba.”
“Sasa kwa nini anakuhofia, si afanye mwenyewe kazi za ndani asiweke msichana.”
Mimi niliguna tu, nikarudi chumbani.
Kusema kweli, maneno ya baba Jamila yalinipa nguvu. Kwamba nimzoee tu mama Rehema. Kwa hiyo nilibatilisha uamuzi wangu wa kutaka kuondoka, nikaenda dukani kununua dawa na kumletea mama Rehema…
“Mbona umechukua muda mrefu, ulipitia kwa wanaume siyo?” alisema kwa ukali…
“Hapana mama. Dukani palikuwa na wateja wengi.”
“Halafu wewe mama Rehema, yaani kumtuma dukani mtu kuchukua dakika kumi tu, tayari alipitia kwa wanaume? Mbona huyu Jamila bado mgeni sana, anaweza kuwa ameshaanza mambo ya wanaume kweli?”
“Eee…hivi wewe baba Rehema na Jamila kuna nini katikati yenu? Kila nikimsema vibaya wewe unapinga, unatakaje sasa?”
“Nataka uwe unamsema vizuri,” alisema baba huku akisimama na kuingia chumbani.
Nilikwenda kulala. Usiku kwangu ulikuwa mzito kila nikimfikiria mama Rehema maana tangu nimeanza kazi kwake hajawahi kunichekea hata siku moja! Basi hata asicheke atabasamu tu lakini wapi!
***
Siku hiyo niliwahi sana kuamka, nikaamua kuanza na sebuleni kwanza kwa kufuta madirisha, tivii, redio, kila kitu. Akaja mama Rehema…
“Mbona umewahi sana kuamka, unamsubiri nani hapa sebuleni?”
“Shikamoo mama,” mimi niliamua kuanza kwa salamu kwanza kabla ya kumjibu…
“Kula mwenyewe hiyo shikamoo yako kama ni mali sana,” ndivyo alivyonijibu.
Mara baba Rehema naye alitokea chumbani…
“Shikamoo baba,” nilimsalimia…
“Wewe, si nimekwambia kula mwenyewe shikamoo zako,” alisema mama, baba akabaki amesimama akishangaa, akamuuliza…
“Mama Rehema una maana gani kumwambia Jamila ale shikamoo zake wakati amenisalimia mimi?”
“Kwani mpaka akusalimie?”
“E! Ina maana Rehema akiamka asiponisalimia nione ni kawaida tu mama Rehema?”
Mama Rehema alibaki kimyaaa! Baba Rehema akaenda bafuni, nikakumbuka sijaweka maji…
“Mama sijaweka maji ya kuoga, mwambie baba.”
“Kamwambie mwenyewe. Kwanza kwa nini usiweke maji? Mimi ndiyo nikufanyie kazi zako siyo?”
“Nilijua nitaweka mama,” nilimjibu huku nikienda chooni…
“Jamila maji hakuna.”
“Naweka baba, nisamehe sana.”
“Usijali, weka.”
Baba alisimama kwenye mlango wa bafuni, nikachota maji na kuingiza bafuni, wakati natoka ili yeye aingie akanishika mkono na kuniita kwa sauti ya chini sana…
“Jamila…”
Je, nini kitaendelea? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.