×

Matumizi yako yanavyoweza kukukwamisha!

WAPO watu ambao kila siku wanalalamika maisha kwao ni magumu, kila kitu hakiendi n.k. Lakini pia kuna wale ambao ni mabingwa wa kulalamika kuwa hawana bahati au mambo yao hayawakalii vizuri.

Lakini wakati wakiwa kwenye mawazo hayo, hawana muda wa kujichunguza na kufuatilia kila shilingi inayoondoka kutokana na mitindo yao ya maisha.

Ndugu zangu, upo uhusiano mkubwa sana kati ya mafanikio na matumizi yako, hasa yale ya kawaida ambayo umezoea kuyafanya kila siku. Lazima ujiulize, je, unatumia fedha zako sawasawa?

Kila fedha yako inayotoka, inakuwa na sababu za msingi au unatumia kwa sababu tu zipo mfukoni mwako? Fedha inahitaji nidhamu ya hali ya juu. Ukiitumia kwa fujo au bila mpangilio kwa sababu tu unayo mfukoni, mafanikio kwako yatakuwa ndoto za mchana.

Baadhi ya watu wanatumia fedha nyingi sana, lakini kwa sababu hawana utaratibu wa kuweka rekodi, mwisho wa siku wanajikuta wametumia nyingi bila kujua na wanabaki katika maisha yaleyale siku zote.

Huwezi kufanikiwa kwa kuwaza fedha nyingi kwa mara moja. Huwezi kupata fedha nyingi kwa mara moja kabla hujashika kidogo kwanza. Swali la msingi ni je, hicho kidogo unachokipata unakitumiaje? Ukishindwa kutumia kidogo kwa nidhamu, hakika hata ukipewa kikubwa, hutaweza kukitumia sawasawa, badala yake utaishia kulalamika kila siku kuwa maisha ni magumu.

Je, wewe unaishije? Mambo yako yakoje? Unajihisi huna fedha kwa ajili ya mipango mikubwa ya maisha yako? Anza na kuangalia matumizi yako ya kawaida ya kila siku.

Ukituliza akili utagundua kuna mahali huwa unafanya makosa makubwa sana ambayo yanagharimu maisha yako. Hebu anza na matumizi yako kwanza.  

USAFIRI

Kuna watu maisha yao ni ya kawaida, labda anafanya kazi lakini mshahara wake ni wa kawaida kabisa ambao katika hali ya kawaida hautoshi kununua usafiri wake hivyo anatumia usafiri wa jumuiya.

Tatizo ni aina gani ya usafiri unatumia? Sasa mwingine utakuta anataka kukodisha taksi, bajaj au bodaboda wakati mfuko wake hauruhusu. Acha kuishi kwa mazoea, angalia hiyo 1000 unayoidharau na kumlipa bodaboda, ukihifadhi kwa mwezi utakuwa na kiasi gani?

Mwingine anaishi labda Mbezi kwa mfano, ameshuka kwenye daladala na anapokwenda si mbali, lakini analazimika kukodisha bodaboda, ya nini? Kwanza jioni ndiyo kwanza unarudi nyumbani, haraka ya nini? Tembea kwa miguu yako.

Ninachotaka kusisitiza hapa ni kwamba hakikisha unapoamua kukodisha usafiri basi uwe na sababu za msingi kama kuwahi mahali fulani au vinginevyo. Siyo kutumia usafiri wa kukodisha katika mazingira ambayo yatakuumiza tu, lakini sababu za msingi unakuwa huna.

CHAKULA

Acha tabia ya kuingia kwenye mgahawa kisha ndiyo ujue utakula nini. Weka bajeti yako ya kula mchana ukiwa kazini mapema. Kichwani uwe unajua kabisa kuwa mchana utatumia 3000 (labda) na isitokee ukaingia na kutamani kula wali kuku ambao ni 5000 wakati bajeti yako ni 3000 tu.

Nidhamu hii itakusaidia kutunza fedha zako, badala ya matumizi ya ghafla ambayo hayakuwa kwenye ratiba.

ANASA

Kwa kawaida binadamu tunapenda vitu vizuri, lakini angalia mfuko wako kwa sasa unaruhusu? Kuna ulazima gani wa wewe kunywa pombe kupitiliza? Mwingine kila siku anakuwa baa au kwenye kumbi mbalimbali za starehe. Je, umeshapima ukajua unatumia kiasi gani?

Pamoja na kwamba moyo unapenda vitu vizuri lakini ni afadhali ujinyime kwa muda ili baadaye ukipata fedha nyingi, ndiyo unaweza kuishi maisha utakayoyachagua.

FANYA HESABU

Pengine bado unaona ugumu wa kuachana na matumizi yasiyo ya msingi ambayo yanakurudisha nyuma. Ili iwe rahisi kwako kuelewa somo hili, fanya kitu kimoja; weka rekodi.

Andika kila unachotumia kila siku. Mfano asubuhi umechukua bodaboda, mchana umekula, vocha labda na bia nne, tano na marafiki jioni. Andika zote na uwe kumbukumbu mahali. Baada ya mwezi mmoja rudi pale ulipoandika na upige hesabu.

Bila shaka utagundua namna unavyofuja fedha na utabadilika kuanzia siku hiyo.

Leave a Comment