Said Ally, Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, amewapa kazi maalum wachezaji wa kikosi hicho kuhakikisha wanafanikiwa kupata bao la kuongoza ndani ya dakika 15 tu watakapovaana na timu ya Cercle de Joachim ya Mauritius katika mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga wanatarajia kuondoka nchini leo Jumatano kuelekea Mauritius kukipiga katika mchezo wa awali mkondo wa kwanza ugenini wikiendi hii.
Pluijm alisema lengo kubwa ya mbinu hiyo ya kutaka bao la kuongoza ndani ya dakika 15 za mwanzo ni kuwachanganya wapinzani wao ambao watafunguka kusaka bao la kurudisha na kuwapa wao nafasi ya kufunga mabao mengine zaidi.
“Lengo letu la kwanza ni kuhakikisha tunashinda mchezo wetu huu wa ugenini lakini kitu cha muhimu ni kuhakikisha tunapata bao la kuongoza katika dakika za mapema kwani kwa kufanya hivyo, tutapunguza presha ya mchezo.
“Lakini kupitia bao hilo, tutawafanya wapinzani wetu wachanganyikiwe, hivyo watafunguka ili kutaka kurudisha bao hilo na hivyo nafasi hiyo itatupa sisi mwanya wa kuweza kuongeza bao lingine.
“Tutacheza kwa tahadhari ya hali ya juu ambapo tutatumia mfumo wa kushambulia zaidi na kujilinda tusifungwe kwani kama unavyojua mbinu nzuri ya kujilinda katika mechi ni kumshambulia mpinzani wako,” alisema Pluijm.
Kazi hiyo ya kushambulia, itaongozwa na wafungaji hatari Amissi Tambwe na Donald Ngoma ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa kwenye timu hiyo.