
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeshtushwa na kitendo cha kukamatwa kwa aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, kikidai kuwa taratibu za kisheria hazikufuatwa.
LHRC imeeleza kuwa ukamataji huo umefanyika bila taarifa rasmi za sababu za kukamatwa kwake kutolewa, hali inayokiuka haki za msingi za kikatiba na utawala bora.
Katika tamko lake, LHRC imekemea vitendo vya ukamataji usiofuata taratibu, ikibainisha kuwa matukio kama haya yamekuwa yakiongezeka, jambo ambalo linahatarisha haki za raia na uhuru wa kujieleza.
“Tanzania ni nchi ya kidemokrasia ambapo kila raia ana haki ya kuishi kwa amani na kujieleza bila hofu. Matukio ya ukamataji kiholela yanaashiria udhaifu katika uzingatiwaji wa utawala wa sheria nchini,” alisema Dkt. Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC.
LHRC pia imeitaka serikali na vyombo vya dola kueleza kwa uwazi tuhuma zinazomkabili Boniface Jacob ili kuepusha upotoshaji unaosambazwa mitandaoni kwamba alitekwa nyara.
Dkt. Henga aliendelea kusema, “Haki ya kutambua sababu ya kukamatwa ni ya msingi katika mchakato wa haki, na kukamatwa kwa siri au bila uwazi kunahatarisha uaminifu wa raia kwa vyombo vya dola.”
Kwa upande mwingine, LHRC imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu, haki ya usawa mbele ya sheria, na uwajibikaji wa vyombo vya usalama.
Katika tamko la awali, Jeshi la Polisi kupitia kwa msemaji wake DCP David Misime lilithibitisha kumkamata Boniface Jacob kwa tuhuma za kijinai, likiwataka wananchi kupuuza uvumi wa mitandaoni kwamba ametekwa. Hata hivyo, LHRC imeendelea kusisitiza kuwa kitendo cha ukamataji kinapaswa kufanywa kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya kisheria ili kuepusha malalamiko na migogoro isiyo ya lazima.
