×

Mikoa, Halmashauri Zaagizwa Kushiriki Maonesho Ya Viwanda

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameagiza mikoa na hamlashauri zote nchini kuhakikisha viwanda vilivyo katika mamlaka zao vinashiriki katika maonesho ya biashara ya kimataifa.

Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 26, 2024 Jijini Dar es salaam wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango katika ufunguzi wa Maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Viwanda Tanzania mwaka 2024.

“ Naagiza Mikoa na Halmashauri zote nchini kuhakikisha Viwanda vilivyo katika Mamlaka zao vinashiriki kuonesha bidhaa wanazozalisha ili bidhaa hizo ziweze kutafutiwa masoko ya ndani na nje ya nchi yakiwemo ya ukanda wa EAC na SADC kwa lengo la kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma za Tanzania nje ya nchi,” amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji hususani katika sekta ya viwanda ili kukuza uchumi wa Viwanda na nchi kwa ujumla.

“ Tutakumbuka kuwa andiko letu la Blueprint ambalo limeainisha changamoto mbalimbali zinazokwaza maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara nchini na mapendekezo ya nini kifanyike ili kuondoa changamoto hizo. Kazi hiyo ilianza katika Awamu ya Tano na nipende kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuhakikisha kuwa changamoto zinazoikabili biashara na uwekezaji ikiwemo katika sekta ya viwanda zinaendelea kutatuliwa.” Amebainisha Dkt. Biteko.

Aidha, amewahamasisha wafanyabishara na wenye viwanda nchini, kuendelea kushirikiana na Serikali na Taaasisi zake, katika kuhakikisha kuwa changamoto zinazoikabili sekta ya viwanda nchini tunazitatua kwa pamoja ili kukuza uchumi wa nchi.

MAMA LOVE KUNGWI AKATAA KUWA SHANGINGI – “HATUPENDI WANAUME BARIDI – TUNAPENDA wa MOTO”…

Leave a Comment