
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amefanya ziara ya kikazi mkoani Tabora tarehe 8 Oktoba 2024 na kuzindua mradi wa upanuzi wa maji ya Ziwa Victoria.
Mradi huo una gharama ya shilingi bilioni 29.3 wenye ujazo wa maji laki 9 kwenye matenki 7 ambapo utahudumia wananchi 82,000 wa Kata ya Bukene; ikiwa ni pamoja na Kata za jirani za Mwamala, Itobo, Isanzu na Ikindwa.
Sambamba na hilo, Makamu wa Rais pia amezindua mradi wa maji taka wenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 katika Wilaya ya Nzega.
“Nipongeze wananchi wa Tabora kwa kazi nzuri lakini nitoe msisitizo kwenye uharibifu wa mazingira mnakata sana miti, Lakini tuna nafasi ya kurekebisha hilo kwa kupanda miti kila kaya miti 3 na ata wanafunzi wanaweza nao kupanda kila mmoja wao,” amesema Makamu wa Rais Mhe. Mpango.

Amehamasisha pia wananchi kupeleka watoto shule ili kuwekeza kwenye taaluma itakayopatikana; na kuongeza lishe bora kwa watoto. Vile vile, kutumia nishati safi kwa kuwa kuni na mkaa zinaumiza watoto wa kike.
Alipongeza hatua ya Wizara ya Kilimo kupeleka matrekta 40, vituo vikubwa vya zana za kilimo, maafisa ugani, pikipiki, baiskeli, kujenga maghala, kutoa mashine za kukoboa mpunga katika kusaidia wakulima wakiwemo wa tasnia ya Pamba.

Ziara hiyo imeshirikisha pia Viongozi mbalimbali akiwemo Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo ambaye ni Mbunge wa Nzega Mjini. Wakati akisalimia wananchi, Waziri Bashe alitoa shukrani kwa ujio wa Makamu wa Rais na uwezeshwaji wa fedha mbalimbali zilizotolewa na Mhe. Rais Dkt. Samia katika kukuza hali ya uchumi kwa wananchi wa Nzega na Mkoa wa Tabora kwa ujumla.
Alimtaarifu Makamu wa Rais kuhusu ziara yake ya Mkoa wa Tabora mapema mwezi Septemba 2024 na kueleza maelekezo ya Serikali ya kuanza kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao ya choroko, dengu, mbaazi na jamii ya mikunde ili kuepuka wizi na madalali wanaoumiza wakulima.