
Bunge la seneti nchini Kenya, baadaye leo jioni linatarajiwa kupiga kura ya ndio au la, ya kumuondoa ofisini Naibu Rais, Rigathi Gachagua, baada ya kuskiza hoja ya matumizi mabaya ya afisi ambayo tayari imeidhinishwa na bunge la kitaifa.
Gachagua anakabiliwa na mashtaka 11 ya matumizi mabaya ya afisi ikiwemo rushwa, kueneza siasa za kikabila na kuhujumu serikali.
Baada ya mashahidi wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wao hapo jana katika kikao kilichojawa majibizano makali kutoka kwa mawakili, hii leo itakuwa zamu ya Naibu Rais Rigathi Gachagua maarufu kama “Riggy G” kujitetea mbele ya maseneta.
Gachagua amekanusha mashtaka yote dhidi yake, akisema yamechochewa kisiasa baada ya uhusiano kati yake na rais William Ruto kudaiwa kuingia doa, hata hivyo huenda akaondolewa afisini iwapo bunge la Seneti litaidhinisha mashtaka dhidi yake.
Aidha naibu huyo wa rais atakuwa na fursa ya kujieteta mahakamani iwapo ataondolewa ofisini na bunge.