
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema ameahirisha mpango wa kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran baada ya kushauriwa na viongozi wa Qatar, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu (UAE), ambao walimtaka ape nafasi zaidi kwa njia ya diplomasia badala ya vita.
Akizungumza akiwa ndani ya ndege ya Air Force One, Trump alisema jeshi la Marekani lilikuwa limeandaa kile alichokiita shambulio kubwa zaidi tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, lakini aliamua kulisitisha baada ya mazungumzo na viongozi wa Ghuba, akiwemo Mohammed bin Salman.
“Niliuliza Mwana Mfalme, ‘Ungependa tufanye mashambulizi au la?’ Walisema wangependelea makubaliano kuliko mashambulizi kwa sababu hujui vita vinaweza kuishia wapi,” alisema Trump.
Trump alitangaza kuwa mazungumzo mapya kati ya Marekani na Iran yataanza Jumatatu, yakilenga kumaliza vita vilivyoanza miezi mitano iliyopita. Alisema ajenda kuu zitakuwa hatma ya Strait of Hormuz pamoja na mpango wa kuiondolea Iran uwezo wa nyuklia.

Kwa upande wake, Iran imesema iko karibu kufikia makubaliano na Oman kuhusu njia mpya ya usafiri katika Mlango wa Hormuz, huku ikisisitiza kuwa hatua hiyo haimaanishi kufunguliwa tena kwa njia hiyo muhimu ya kimataifa.
Tangazo la Trump lilichangia kushuka kwa bei ya mafuta katika masoko ya Asia, ambapo mafuta ghafi aina ya West Texas Intermediate (WTI) yalishuka kwa asilimia 4.7 hadi dola 80.72 kwa pipa.
Marekani na Iran zimekuwa katika mgogoro wa kijeshi tangu Februari 28, baada ya Marekani na Israel kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran. Hata hivyo, juhudi za kidiplomasia zimekuwa zikiendelea huku pande zote zikitafuta njia ya kumaliza mzozo huo.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Iran vimekanusha madai kwamba Tehran iliomba Trump asifanye mashambulizi, vikisisitiza kuwa hakuna ombi rasmi lililotolewa kwa Marekani.