×

Maelfu Wafaidika na Mradi wa Panda Miti Kibiashara

Maelfu ya wananchi wamenufaika na Mradi wa Panda Miti Kibiashara Awamu ya Pili (PFP2) ambao umewezesha kukuza upandaji miti endelevu na shirikishi unaochangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania na kupunguza umaskini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Mradi huo akiwa na Mwenyekiti Mwenza Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Theresa Zitting, leo Oktoba 24, 2024 wakati wa kikao cha mwisho cha mradi huo unaofadhiliwa na Serikali za Finland na Tanzania.

“Mradi huu umekuwa muhimu na bado utakuwa muhimu sana katika sekta ya misitu, hasa katika kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza ushiriki wa wananchi kwa ujumla katika usimamizi wa misitu. Msaada huo mkubwa wa PFP na Serikali ya Finland umewezesha maelfu ya wananchi wa Iringa na Njombe kupanda miti kibiashara na kujiongezea kipato,” amesema Dkt. Abbasi.

Amesema mradi huo kwa kiasi kikubwa umefanikisha upandaji wa miti katika mashamba yenye ukubwa wa hekta 250,000 yanayomilikiwa na wananchi wenyewe ikiwa ni idadi kubwa zaidi kushinda shamba kubwa la Serikali la Sao Hili ambalo sehemu ya upandaji miti ni hekta 86,003 pekee na ndilo chanzo kikuu cha miti na mbao hapa nchini.

Dkt. Abbasi ameishukuru timu ya PFP na Balozi wa Finland kwa kazi nzuri waliyofanya katika kutekeleza mradi huo muhimu na maalum zaidi kwa jamii zilizokubali kufanya kazi na timu ya mradi.

Pia ameahidi kuhakikisha kuwa kunakuwa na mipango ya kuendeleza mafanikio ya mradi huo na wakati mwingine kuiga vitendo hivyo vya mafanikio katika maeneo mengine nchini.

Kikao hicho kimefanyika katika Chuo cha Viwanda na Misitu Mafinga ambacho nacho sasa kilikiwa cha muda ila kimenunuliwa na kitaendelezwa na Serikali ili kuwapatia vijana ujuzi wa sekta ya misitu.

Leave a Comment