
Kiungo mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania na Klabu ya Soka ya Azam FC, Feisal Salum ‘Feitoto’ (26), amekataa kuzungumzia tetesi za usajili zinazoendelea zikimuhusisha na Klabu ya Simba SC pamoja na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Feisal Salum baada ya kuisaidia timu yake kupata ushindi wa 3-1 hapo jana dhidi ya Dodoma Jiji, akifunga bao moja na kutoa pasi ya usaidizi wa bao (asist), baada ya mchezo alipoulizwa kuhusu hatima yake baada ya mkataba wake kumalizika, alikataa kuzungumza ni wapi ataelekea huku akisisitiza kuwa yeye bado ni mchezaji wa Azam FC.
Feisal Salum amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake ndani ya Azam FC, tetesi nyingi zinamhusisha kujiunga na wababe wa Kariakoo Simba SC, huku zingine zikimuhusisha kuhitajika na kocha wake wa zamani Nesredine Nabi anayeinoa Klabu ya Kaizer Chiefs kule Afrika Kusini.
Mpaka Sasa Feisal Salum amechangia mabao tisa msimu huu, akifunga mabao manne na kutoa pasi tano za usaidizi wa mabao na kuisaidia timu yake kushika nafasi ya kwanza katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC, ikiwa na alama 30 baada ya michezo 13 alama mbili zaidi ya mnyama Simba, mwenye alama 28 katika nafasi ya pili baada ya michezo 11.