
KIKOSI cha Yanga kinaondoka leo Jumanne kuelekea Algeria lakini tayari kimetanguliza watu wao wawili kwenda kuweka mambo sawa. Taarifa za ndani zinasema tayari Hafidhi Saleh ambaye ni mratibu wa timu amewasili Algeria akiwa na Mkurugenzi wa Mashindano wa klabu hiyo, Ibrahim Mohamed.
“Kule ni ugenini hivyo viongozi waliokwenda watakuwa na kazi ya kufanya maandalizi yote ya wapi timu itafikia na mambo mengine kama usafiri na kadhalika. Sababu ya pili wamepata taarifa kuwa mechi inaweza kuhamishwa uwanja, hivyo wamefika kupata uhakika na kujua timu itafika wapi kama uwanja utabadilishwa,” kilisema chanzo.
Hata hivyo, uamuzi wa MC Alger kutaka kubadilisha uwanja unaweza usiwasumbue sana Yanga kwani wapinzani wao wana marufuku ya mechi nne za Caf nyumbani kucheza bila ya mashabiki. MC Alger imetakiwa kucheza mechi nne za nyumbani za michuano ya Caf bila ya mashabiki kutokana na utovu wa nidhamu waliouonyesha mashabiki wao katika mchezo wa mwisho wa kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo msimu huu katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya US Monastir.
Rais wa MC Alger, Mohamed Hakim amesema klabu hiyo imepeleka barua Caf; “Barua yetu imepokelewa na Caf na upo uwezekano mechi yetu dhidi ya Yanga ikahamishiwa kuchezwa uwanja wetu wa Ali la Pointe, zipo sababu za msingi sisi kuwasilisha ombi hilo, tunataka mechi hii iwe na mvuto pande zote, watu wafurahie mpira zaidi.