ILIPOISHIA:
Imbori akiwa amechanganyikiwa kutokana na kupotea ghafla kwa Bayo, Dickson anapigiwa simu na mkuu wa polisi kutoka kituoni Compton aliyemuuliza ikiwa anafahamiana na kijana huyo jambo alilolikanusha, lakini taarifa hizo zilimshitua sana Dickson na hakupenda kabisa kuamini kuwa Bayo alikuwa hai wakati huo.
TeRemka nayo…
KAMA ilivyokuwa kwa Dickson, Benson MacKenzie pia alijikuta akiingiwa na maswali mengi juu ya taarifa ya kuonekana kwa Bayo.
Alijiuliza ni muujiza gani ulitokea mpaka Bayo kupona, lakini hakupata jibu. Aliamua kuwashirikisha wenzake lakini wao pia walikataa katakata kuwa Bayo alionekana. Waliamini lilikuwa ni jambo lisilowezekana kwake kupona.
Lakini ukweli ni kwamba vijana hao walikuwa wanabisha juu ya jambo ambalo walikuwa hawalifahamu. Katika purukushani za kumbeba Bayo na kwenda kumfungia katika chumba walichoamini asingefanikiwa kutoroka ili walichome moto jumba hilo, kamba walizokuwa wamemfunga mkononi zililegea.
Hiyo ndiyo ikawa fursa kwa Bayo kuitumia kujifungua kamba zote alizokuwa amefungwa miguuni mwake punde tu alipofungiwa kweye chumba hicho.
Baada ya kufanikisha hilo hakupenda kupoteza muda maana aliwasikia wakiongea kwa Kiingereza kuwa wafuate madumu ya petroli na kumchomea ndani, hivyo kwa kutumia dirisha lililokuwa wazi Bayo alitoka nje ya chumba hicho. Kwa ujasiri na tahadhari kubwa akajivuta hadi ilipokuwa fensi ya jengo hilo.
Kwa hiyo wakati akina Benson wanalilipua kwa moto, ndipo Bayo alikuwa katika harakati za kuruka upande wa pili, jambo ambalo alifanikiwa bila moto kumdhuru kwa kiasi kikubwa. Hakuna mtu yeyote kati ya maharamia hao aliyefahamu kuwa Bayo alifanikiwa kutoka akiwa mzima wa afya!
Bayo alisimama umbali wa mita 20 akilishuhudia jengo hilo likiteketea kwa moto. Moyo ulimuuma mno kiasi kwamba machozi yakaanza kumbubujika bila kuelewa. Tukio hilo kwake lilikuwa fundisho kubwa sana lililomfanya atambue juu ya uwepo wa Mungu na rehema zake.
Hakupenda kupoteza muda akiwa katika eneo hilo, aliamua kuondoka huku akiwa na malengo ya kwenda kwenye kituo cha polisi kilichokuwa karibu kuripoti kilichotokea. Baada ya kuulizia kwa wakazi wa eneo alilokuwepo alifanikiwa kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Compton alikotoa maelezo.
Hatimaye siku hiyo ikayoyoma. Siku ya pili yake baada ya Dickson kufahamishwa juu ya mashitaka yake na kesi kufunguliwa mahakamani ikasikilizwa kwa muda wa miezi miwili, alipatikana na hatia. Mahakama ikamhukumu yeye na akina Benson kifungo cha maisha jela.
Hizo zilikuwa ni taarifa zilizomsikitisha kila mtu aliyemfahamu Dickson kama ilivyokuwa kwa Josephine, lakini hakukuwa na namna tena ya kumnasua katika kitanzi hicho. Sheria ilichukua mkondo wake na Imbori alikabidhiwa kwa Bayo.
“Asante mpenzi!” Imbori alimwambia Bayo akimtazama machoni.
“Kwa lipi?”
“Kunipigania.”
“Ilinibidi kufanya hivyo.”
“Ni kweli kabisa, lakini ni kwa sababu unanipenda kwa dhati.”
“Hujakosea, hakuna wa kunitenganisha na wewe.”
“Asante.”
Wawili hao walikumbatiana kwa furaha huku machozi yakiwabubujika, baada ya kuachiana walipanda kwenye gari la polisi wakapelekwa hadi kwenye ubalozi wa Tanzania nchini Marekani kwa ajili ya kusafirishwa kurudi Tanzania.
Taratibu zote za safari zilifanyika, baada ya kumalizika Bayo na Imbori wakapanda ndege ya Shirika la Kermo iliyotakiwa kuwasafirisha hadi Algeria ili wabadilishe ndege nyingine ambayo wangetua Kenya na kuchukua usafiri mwingine hadi Tanzania.
“Nimepamiss sana nyumbani,” Imbori aliongea huku akimlalia Bayo ndani ya ndege.
“Kumekumiss pia.”
“Kweli?”
“Haswaa!”
“Nashukuru sana Bayo ila kuna kitu bado sijakutendea haki.”
“Kipi?”
“Kwanza kukushukuru juu ya uliyonitendea, lakini pia kukuomba msamaha kwa yote yaliyotokea kati yangu na Dickson.”
“Mbona huchoki kushukuru mpenzi! Nishakusamehe kwa kila kitu, wewe ni wangu daima maana mapenzi yetu yako ndani ya damu.”
Ukweli ni kwamba Imbori alimchukulia Bayo kuwa mwanaume mwenye moyo wa pekee sana duniani, upendo wake ulikuwa ni zaidi ya upendo. Alijifikiria amshukuru kwa namna gani lakini hakupata jibu, kila alichowaza kumfanyia aliona kilikuwa hakitoshi zaidi ya neno asante alilolimaanisha.
Wakati wote huo wa safari Imbori alikuwa anatabasamu tu, hatimaye wakafika Algeria walikobadilisha ndege na kupanda ndege ya Shirika la Emirates iliyowapeleka hadi Kenya walikobadilisha pia kwa kukwea Air Tanzania.
Baada ya saa nyingi za kusafiri kutoka Marekani safari yao ya anga ikakomea kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA). Wakawa wamefika Tanzania walikoanzisha maisha mapya! MWISHO!
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/