×

Nilivyoteseka Kwenye Mianzi ya Kichawi – 8

ILIPOISHIA

“Kila mmoja wenu atapewa nafasi ya kuzungumza na kumwambia mfalme kile alichonacho moyoni.
“Kama unataka kusamehewa utamwambia na utatoa sababu, mnaweza kuiepuka adhabu ya kupoteza maisha iliyopo mbele yenu mkiwa makini kujieleza kwake, kuna mwenye swali?” aliuliza kamanda yule.
“Ndiyo, tunalo,” nikamjibu.
“Uliza, wewe si ndiye kiongozi wa wahalifu hawa?”

SONGA NAYO…

Nauliza, tutakapokutana na mfalme, kila mmoja ataongea kivyake au mimi nitawakilisha wote?”

“Kisheria inatakiwa kila mmoja ajitetee mwenyewe, aeleze matatizo yake ili mfalme aone nani atamsamehe au nani adhabu yake iendelee na sisi huwa tunatekeleza huko kwenye shimo la kifo. Mwingine mwenye swali?”
Kijana mmoja alisimama na kufuta machozi kisha kuuliza: “Kwani tunaweza kutumbukizwa shimoni wote kwa pamoja au mmoja mmoja?”
“Hilo swali lako nikikujibu litakusaidia nini? Uliza maswali ya maana, au hamjanielewa?”
Kimyaa.

Yule kamanda akaendelea: “Nia ya kujieleza ni kupima uzito wa matatizo yenu kwani huwa yanatofautiana. Kwa mfano, msichana anaweza kuwa na ujauzito, akijieleza pale anaweza kusamehewa kwa sababu kisheria mwanamke mjamzito hairuhusiwi kutumbukizwa kwenye shimo la kifo.”
“Kama yule msichana anadanganya?” aliulizwa msichana mwingine.

“Akidanganya atakuwa anajidanganya mwenyewe kwa sababu mimba huwa haitumbukizi tumbo ndani badala yake huwa tumbo linachomoza, hivyo kama atadanganya ni lazima atakuja kujulikana. Umeelewa?”
“Nimeelewa, lakini mtu kama huyo anapewa adhabu gani?”
“Ukijulikana kuwa umemdanganya mfalme, adhabu huwa ni kukatwa kichwa palepale.”
Baada ya kusema hayo niliwaona wasichana wengi wakiinamisha vichwa vyao, bila shaka walitegemea uongo huo kuwaokoa.
Baadaye yule kamanda aliuliza kama kuna mtu mwingine mwenye swali lakini ikaonekana hakukuwa na aliyekuwa na swali pengine watu walikuwa na hofu ya kifo maana dakika zilikuwa zinazidi kusonga mbele.

Msafara ulianza kuelekea kwa mfalme na tulikuwa katika mistari miwili, mmoja wa sisi wavulana na wa pili ulikuwa wa wasichana na wao ulikuwa na watu wasiopungua nane, wetu ulikuwa na watu ishirini na moja.

Safari kuelekea kwa mfalme ilianza kwa mwendo wa taratibu huku tukiongozwa na ngoma iliyokuwa ikipigwa kadiri tulivyokuwa tukipiga hatua na tuliambiwa awali kuwa tufuate mapigo ya ngoma hiyo kubwa ambayo shuleni tulikuwa tukiita mdundo.
Baada ya mwendo wa dakika kumi niliona mbele yangu umati ukiwa umezunguka jukwaa nikatambua kuwa pale ndipo alipo mfalme.

Mawazo yangu yalikuwa mengi kadiri tulivyokuwa tunakaribia umati ule na nikawa najiaminisha kuwa mfalme yupo pale.
Tulipokaribia umati ule, wananchi wenyewe walitupisha njia na baada ya kuacha uwazi nilimuona mfalme akiwa ameshika mkuki wa rangi ya shaba ambao ni ishara ya mamlaka aliyokuwanayo.
Tulisimamishwa mbele yake na ile ngoma iliyokuwa ikipigwa iliacha kuvuma kuashiria tulifika. Tuliambiwa tugeuke kulia ambapo mfalme alikuwa ameketi kwenye kiti chake cha enzi.
Yule Kamanda Ben Mtwanga aliyetuleta pale alimtaarifu mfalme kwamba mbele yake kuna watu ishirini na tisa ambao wamefanya makosa kwenye bustani ya Nangose na wanasubiri amri yake ya kutupwa kwenye shimo la kifo.

Mfalme alisimama na kuanza kusema: “Wananchi wangu kama ilivyo ada kabla ya hawa watu hawajatupwa kwenye shimo la kifo ni lazima niwasikilize utetezi wao wa mwisho wa kwa nini wapunguziwe adhabu. Utetezi huu hufanywa sehemu ya wazi kama hivi.”
“Sawa mkuu. Utaratibu ni kwamba tuanze na kiongozi wao wa msafara Bwana Issa Namakoto,” alisema Kamanda Mtwanga.
“Sawa. Issa Namakoto nenda kasimame pale alipo mfalme ujieleze.”
Nilianza kutetemeka mwili kama vile nina homa kali. Nilikwenda taratibu na kusimama mbele yake, nilihisi nitashindwa kutoa maneno.

“Ehee, adhabu yako ni kutupwa ndani ya shimo la kifo, una utetezi wowote?” Mfalme akaniuliza.
“Ndiyo mfalme mtukufu.”Nilikohoa kidogo ili kuweka sawa sauti yangu, nikaendelea:
“Mimi unayeniona maulana mfalme ni Mtume wa Mungu. Sijui katika nchi hii mnajua maana yake.”
“Hatujui na mimi binafsi sijui.”
“Mtukufu mimi nina uwezo wa kufanya mengi ambayo binadamu hawezi kwa mfano naweza kumchinja mtu kisha nikarudishia kichwa chake kwenye shingo yake na akawa hai tena kama kawaida.”
Baada ya kutamka hayo nilimuona mfalme akiwageukia wasaidizi wake akawauliza:
“Ni ya kweli hayo?”
“Hatujui maulana.”
“Hebu fanya tuone.”
Nilimuita kijana mmoja aitwaye Chambilecho ambaye tulikuwanaye katika msafara wetu na tumekuwa tukifanya naye mchezo huo wa mazingaombwe mara nyingi.
Nilifanya mazingaombwe yangu na watu wote pamoja na mfalme wakapigwa na butwaa nikajua kuwa hawa watu wa sehemu hii hawajawahi kuona wala kusikia mambo hayo.
Baadaye nikawaambia nimemchinja rafiki yangu Chambilecho na sasa namrejeshea uhai wake. Nilifanya vitu vyangu na mara akawa mzima.

Nilimuambia arukeruke ili kuthibitishia umma ule kwamba yu mzima, akafanya hivyo na kuzidi kushangaza watu.
Niliomba yaletwe maji kwenye mitungi, nikafanya mazingaombwe na maji yale yakawa divai tamu, niliwaambia watu wainywe, wakainywa na kuzidi kushangaa huku wengine wakisema hakika huyu ni nabii.

Kama vile hiyo haitoshi, nilimchukua ndege na kumuweka kwenye kopo na wote wakashuhudia nikilipondaponda lile kopo lakini nilipofunua kikapu kilichozibwa juu ili ndege asiruke alikutwa mle akiwa hai. Watu walipigwa na butwaaa na kusema mimi ni nabii kweli na kwamba nikitupwa kwenye shimo la kifo, nchi itatikisika.
Mfalme alisimama akautazama umati uliokuwa ukinishangaa huku wengine wakisema sikuwa mtu wa kawaida.
“Sikilizeni,” yule mfalme akaanza kuhutubia.
“Katika maisha yangu sijaona mambo ya ajabu kama haya.”
Je, Namkoto na wenzake watasalimika kutupwa shimoni? Fuatilia hapahapa Jumanne ijayo.

Leave a Comment