Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.
Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.
Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.
Baadaye Magesa anagundua kwamba Grace ni jasusi wa kimataifa, akiwa amebadilisha jina na mwonekano wake, jambo linalompa hofu kubwa ndani ya moyo wake. Hata hivyo, msichana huyo anamuelewesha hali halisi.
Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi. Tayari baadhi ya mambo yameanza kufichuka ambapo inaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya kifo cha Mwampashi na Magesa.
Kaburi ambalo kila mtu anaamini kwamba ndipo alipozikwa Magesa, linafukuliwa na sampuli zinachukuliwa kwa ajili ya vipimo vya DNA. Baadaye inabainika kwamba aliyezikwa hakuwa Magesa bali mtu mwingine tofauti kabisa.
Kadiri upelelezi unavyozidi kupamba moto ndivyo mambo mengi yanavyozidi kuibuka na sasa watu wengine wanahojiwa kuutafuta ukweli wa tukio zima. Sekretari wa Magesa na yule wa waziri mkuu nao wanahojiwa.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
“Kwa hiyo unataka kutuambia kwamba hujawahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Magesa wala hajawahi kukupa ujauzito?”
“Wala, kwanza hajawahi hata kunitamkia mambo ya mapenzi, tulikuwa tunaheshimiana sana.”
“Kwa hiyo hujawahi kumtumia meseji yoyote ya kimapenzi?”
“Sijawahi jamani, Mungu wangu shahidi yangu.”
“Hebu tazama kule kwenye skrini,” alisema Mandiba huku akiwapa ishara wale watalaamu wa teknolojia ya mawasiliano. Muda mfupi baadaye, meseji iliyotumwa kutoka kwenye simu ya mkononi ya msichana huyo, kwenda kwenye namba ya Magesa ilionekana kwenye skrini kubwa ukutani. Watu wote wakaanza kuisoma huku msichana huyo akiwa amepigwa na butwaa, akiwa ni kama haamini.
“Hapana! Haiwezekani! Haiwezekani…” alisema Judith huku akijiziba mdomo kwa kutumia mikono yake yote miwili.
“Hii namba iliyotuma meseji unaifahamu?”
“Ndiyo, ni namba yangu ya simu.”
“Namba ya mtu aliyetumiwa meseji unaifahamu?”
“Ndiyo naifahamu. Ilikuwa ni ya marehemu bosi wangu lakini…”
“Binti hebu usitupotezee muda. Mbona unabisha vitu ambavyo vipo wazi kabisa?”
“Jamani mimi sijawahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Magesa wala sijawahi kumtumia meseji kumwambia kwamba mimi nina mimba yake. Huo ni uongo mtakatifu.”
“Sasa kama ni uongo, unafikiri nani anayeweza kuutunga uongo huu wakati inaonesha kabisa kwamba namba iliyotumika ni yako? Kizuri zaidi mpaka tarehe na saa uliyotuma inaonekana.”
“Sikatai kwamba namba siyo yangu lakini sijawahi kutuma meseji ya aina hiyo kwa bosi wangu hata mara moja. Namheshimu sana mkewe, nisingeweza kufanya kitu kama hicho,” alisema msichana huyo huku akianza kuangua kilio kwa nguvu.
“Kwani hiyo simu unatumia na nani?”
“Natumia peke yangu, huwa sichangii simu na mtu.”
Baada ya jibu hilo, Mandiba na wenzake walitazamana na kupeana ishara ambayo waliielewa wenyewe bila msichana huyo kujua walimaanisha nini.
Askari wawili wakaingia na kumtoa msichana huyo huku akitakiwa pia kukabidhi simu yake, kama ilivyokuwa kwa mke wa Magesa, naye alipelekwa kwenye chumba kingine cha vioo ambacho kilimfanya yeye asione chochote kilichokuwa nje lakini watu waliokuwa nje walikuwa na uwezo wa kumuona. Wakawa wanaendelea kumfuatilia kwa makini kutaka kujua kama kuna jambo alikuwa analificha.
Wakati jopo la wataalamu wengine wakiendelea kuwafuatilia kwa kina, Vivian, mke wa Magesa na Judith waliokuwa kwenye vyumba maalum vya vioo, iliwadia zamu ya mtu wa tatu kuhojiwa, Coletha ambaye alikuwa sekretari wa waziri mkuu ambaye kwa mujibu wa Vivian, simu yake ndiyo iliyotumika kutuma picha za utupu za Magesa akiwa na mwanamke mwingine gesti kwenda kwenye namba ya mkewe.
“Jitambulishe wewe ni nani na unafanya kazi wapi.”
“Naitwa Coletha Magwaza, nafanya kazi Ofisi ya Waziri Mkuu nikiwa kama katibu muhtasi wake.”
“Kwa lugha nyepesi wewe ni sekretari wa mheshimiwa waziri mkuu, si ndiyo?”
“Ndiyo mzee.”
“Hebu tueleze, unamfahamu vipi Magesa?”
“Magesa yupi? Marehemu?”
“Ndiyo!”
“Alikuwa rafiki mkubwa wa bosi wangu. Nakumbuka mara kwa mara nilikuwa nikitumwa kupeleka zawadi mbalimbali ofisini kwake na wakati mwingine nyumbani kwake. Hata yeye alikuwa akija mara kwa mara ofisini kuonana na waziri mkuu kwa hiyo mimi ndiyo nilikuwa nampokea.”
“Uhusiano wako na mkewe upoje?”
“Kama nilivyokuwa namheshimu Magesa, namheshimu pia Vivian, nilitokea kuwazoea wote na kuwapenda.”
“Unaizungumziaje ndoa yao kabla Magesa hajafikwa na mauti?”
“Mh! Ninachojua mimi walikuwa wakipendana sana, kila nilipokuwa nikitumwa kupeleka zawadi nyumbani kwao, nilikuwa nikiwakuta wakifurahi pamoja na watoto wao. Kwa kifupi najua hayo tu.”
“Umewahi kupata taarifa kwamba Magesa alikuwa akiisaliti ndoa yake kwa kutoka na mwanamke mwingine?”
“Hapana! Sijawahi kusikia suala kama hilo hata mara moja.”
“Umewahi kuziona picha za Magesa akiwa na mwanamke mwingine gesti wakiwa watupu?”
“Hapana, sijawahi kuziona,” alisema msichana huyo kwa kujiamini, Mandiba akampa ishara mtaalamu mmoja wa teknolojia ya mawasiliano kisha akamtaka Coletha atazame ukutani kulikokuwa na skrini kubwa.
“Unaijua hii namba?”
“Ndiyo, ni namba yangu ya simu.”
“Na hii nyingine?”
“Mh! Hapana siijui.”
“Huijui kivipi wakati inaonesha simu yako ilituma picha kwenda kwenye hii namba?”
“Picha? Picha gani?”
Kwa kuwa picha zenyewe hazikuwa na maadili, ilibidi ufundi mkubwa utumike kuzionesha upande wa kichwani tu kisha zikarushwa kwenye skrini kubwa, zikiwaonesha Magesa akiwa na mwanamke, wakiwa kitandani.
“Mungu wangu, sijawahi kuziona hizo picha hata mara moja wala sijawahi kumtumia mtu.”
“Binti unajua madhara ya kuzungumza uongo?”
“Nasema ukweli jamani, mimi sizijui hizo picha wala sijawahi kuwasiliana na hiyo namba. Mimi namba zote ninazowasiliana nazo nimezisevu kwenye simu yangu, hiyo siijui kabisa,” alisema Coletha huku akionesha kupatwa na mshtuko mkubwa ndani ya moyo wake.
Ilibidi Coletha naye atolewe na kupelekwa kweye chumba kingine cha vioo, Mandiba na wenzake wakaanza kujadiliana kwa kina juu ya majibu waliyoyapata kwa wote waliowahoji ambapo bado kulionesha kuwa na utata mkubwa juu ya mtu aliyekuwa nyuma ya matukio hayo.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne ijayo kwenye Gazeti la Uwazi.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/
Hadithi nzuri sana napenda nione mwisho wake itakuwaje.