ILIPOISHIA
Ilikuwa ni lazima na mimi niishi humohumo, hata kwenda huko nje, sikutaka kabisa, kama kula, nitakula humohumo, kama kufanya biashara, acha nifanye humohumo, ila kutoka ndani ya kituo cha Ubungo, nisingeweza, kwani hata kama ningetoka, ningekwenda wapi? Sikuwa na sehemu, hivyo kuishi humo niliona kuwa suluhisho. Na humohumo ndipo ningepata huo utajiri.ENDELEA…
Nilipokuwa nikiingia ndani ya kituo hicho, moyo wangu uliniambia kwamba inawezekana nilikuwa peke yangu ambaye sikuwa na makazi, niliamini kwamba unapoingia usiku basi watu wote wangeondoka na kuelekea nyumbani kwao hivyo kubaki peke yangu kumbe kile nilichokuwa nikikifikiria hakikuwa sahihi kabisa.
Muda ulizidi kwenda mbele, ilipofika saa moja usiku, badala ya watu kupungua ndiyo kwanza walizidi kuongezeka. Nilijiuliza kilichokuwa kikiendelea ni kitu gani lakini nikashindwa kufahamu chochote kile. Mabasi kutoka mikoani yaliendelea kuingia kwa zamu, nilichoka sana, nilihitaji kulala lakini sikujua wapi pa kulala kwani kila sehemu niliyoiangalia pale kituoni ilikuwa na mizigo ya watu hivyo kuwa na wakati mgumu.
“Wewe dada!” nilimsikia mwanaume mmoja akiita nyuma yangu, nilipogeuka, macho yangu yakagongana na macho ya mwanaume huyo.
“Abee…” niliitika, akanisogelea.
“Wewe ni mgeni mahali hapa?” aliniuliza huku akiwa amenikazia macho.
“Ndiyo!”
“Umetoka wapi?”
“Morogoro!”
“Unaitwa nani?”
“Naitwa Zakia!”
Kwa jinsi nilivyomwangalia mwanaume yule, nilijua tu kwamba alitaka kunizoea na kulikuwa na kitu kingine alichokihitaji kutoka kwangu. Kiukweli nilifanya mambo mengi mabaya, yasiyopendeza mbele ya jamii lakini wakati mwingine nilitakiwa kuyafanya hayo kwa sababu hali niliyokuwa nayo kipindi hicho, ilinilazimu kufanya hivyo.
“Utalala wapi sasa?”
“Sijajua, sina ndugu yeyote yule…” nilimjibu.
Kwanza akaonesha tabasamu pana, lilinishangaza lakini kitu nilichokumbuka, mwanaume huyu alifanya kama alivyofanya Mudi kwamba kama sina ndugu, basi yeye angejifanya ndugu ila mwisho wa siku alihitaji penzi.
Akaniambia twende sehemu kuzungumza, kwanza niliogopa lakini sikuwa na jinsi, ningefanya nini na wakati nilihitaji msaada mkubwa kutoka kwake? Hivyo nikakubaliana naye. Tukaenda sehemu, ilikuwa pembeni ya duka moja la vinywaji, pale niliona kukiwa na mikeka zaidi ya thelathini ikiwa imekunjwa, sikujua ilikuwa ni ya kazi gani.
“Unajua mpango mzima wa kulala humu?” aliniuliza swali.
“Kulala humu? Kwani kuna watu wanalala humu?” nilimuuliza huku nikionekana kushtuka.
“Ndiyo! Wanakodisha mikeka na kulala, saa kumi na mbili wanairudisha..” aliniambia.
“Wanakodisha wapi?”
“Hapa kwangu…ukitaka nitakupa…”
“Wanakodisha kwa shilingi ngapi?”
“Elfu moja, ila wewe, nitakufanyia bure kabisa…” aliniambia.
Jibu lake lilinipa uhakika juu ya kile nilichohisi juu yake. Sikutaka kukataa, nilikuwa na uhitaji mkubwa wa kukaa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuutafuta utajiri hivyo nilikubaliana naye. Akanipa mkeka na kunioneshea sehemu ya kulala, nikaenda, nikautandika na kulala huko.Maisha yangu mapya yakaanza ndani ya kituo hicho, nilishinda nikiwa huko, sikutoka kwani mambo mengine nilikuwa nikiyafanya humohumo ndani. Mwanaume huyo aliyeitwa Dickson akanitafutia biashara ya kuuza magazeti, kweli nikaanza kuifanya na kuingiza kiasi kidogo cha fedha, hichohicho ndicho nilichokitumia kwa matumizi mengine.
Dickson alinionesha upendo wa ajabu, alionekana kuwa miongoni mwa wanaume waliokuwa na uvumilivu mkubwa. Hakuniambia suala lolote la kimapenzi, wakati mwingine nilikuwa nikijiuliza sababu ya yeye kunisaidia, kwa nini mimi? Je, hali ingeendelea hivyohivyo au mwisho wa siku angebadilika.Mwezi wa kwanza ukapita, nilikuwa nikiendelea kuishi ndani ya kituo hicho na kwa kweli sikuwa nimetokea. Ninayokuandikia hapa unaweza ukashangaa lakini ukweli ulikuwa huo. Ulipoingia mwezi wa pili, Dickson akashindwa kuvumilia, akaniambia ukweli kwamba alikuwa akinipenda na alitaka kunioa.
“Kunioa mimi?” niliuliza.
“Ndiyo!”
“Hapana! Haiwezekani…”
“Kwa nini?”
“Dickson, nipo tayari kwako kwa kila kitu isipokuwa mambo mawili tu,” nilimwambia pasipo kumuonea aibu.
“Mambo gani?”
“Sitaki unioe na sitaki uzae nami, ila mengine yote ruksa…” nilimwambia bila kupepesa macho.
Akatabasamu kidogo na kuniangalia kwa macho yaliyoonesha kama mtu aliyetaka nirudie kauli zangu. Hakuniambia kitu zaidi ya kuondoka kuendelea na shughuli zake huku mimi nikiendelea kuuza magazeti.
Ilipofika usiku, akaniita alipokuwa akilala na kunitaka nimpe kampani kwani usiku huo ulikuwa na baridi kali hivyo nikakubaliana naye na kwa mara ya kwanza kukutana naye kimwili. Moyoni sikuumia, sikujuta kwani tangu nimeingia Dar es Salaam ndiye aliyeonekana kuwa msaada wangu mkubwa.
“Zakia…” aliniita kwa sauti ya uchovu.
“Abee mpenzi…”
“Nataka uwe tajiri kama unavyosema, upo tayari?” aliniuliza huku akiuweka mkono kifuani kwangu. Kabla ya kujibu, nikaachia tabasamu pana.
“Nipo tayari!”
“Kweli?”
“Ndiyo mpenzi! Nimesafiri kutoka Morogoro kuja hapa kwa ajili hiyo tu…” nilimwambia.
“Basi subiri..kesho kuna mtu atakuja, mwambie kila kitu,” aliniambia.
“Anao utajiri?”
“Hana ila ukitaka, anakupa?”
“Kweli?”
“Hakika!” aliniambia huku akiongeza tabasamu usoni mwake. Nikawa na uhakika wa kuuupata huo utajiri.
Usiku wa siku hiyo nilikuwa na presha kubwa, sikuamini kilichokuwa kikiendelea kwamba kesho hatimaye ningeonana na mtu ambaye Dickson alikuwa na uhakika kwamba angeweza kunipa utajiri.
Sikujua ungekuwa ni utajiri wa namna gani, sikujua angenipa nini ila kitu nilichokifahamu ni kwamba ningepewa utajiri.
Kesho asubuhi ilipofika, Dickson akaniaga, akaniambia kwamba siku hiyo asingefanya kazi yoyote ile bali anaondoka kwa ajili ya kwenda kumleta huyo mtu, hivyo nikabaki na presha kubwa.
Je, kiliendelea nini? Usikose kufuatia Jumanne ijayo.