×

SmartLab na Climate-KIC Wazindua Rasmi Programu ya Mazingira Nchini Tanzania

Larry Ayo, Mkurugenzi wa Biashara wa SmartLab akizungumza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa programu ya Adaptation and resilience -ClimAccelerator jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam 12 Desemba 2024: Kampuni ya SmartLab ambayo ni kitovu cha ubunifu nchini Tanzania, kwa kushirikiana na EIT Climate-KIC, shirika la ubunifu wa hali ya hewa barani Ulaya, wamezindua rasmi mpango wa kukabiliana na kustahimili mabadiliko ya hali ya hewa ujulikanao kama ‘Adaptation and Resilience ClimAccelerator’.

Hafla hiyo, iliyofanyika katika makao makuu ya SmartLab jijini Dar es Salaam, imeashiria kuanza rasmi kwa awamu ya pili ya mpango huo unaolenga kukuza suluhisho la kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini Tanzania.

Mpango huu ulipokea maombi ya wajasiriamali zaidi ya 170 kutoka mikoa ya Iringa, Arusha, Dodoma, Zanzibar, Mwanza, na Singida. Baada ya mchujo, wajasiriamali 10 walichaguliwa, wakiwemo, Tanzania Viable Farms, HERVEG.05, NDUGUNAMITI ENTERPRISES LTD, Kilimomax Solutions, insect Up, Rada 360 Limited, THORNTSORN, Kesho Technologies Company Limited, DMA, na Addrone Digital. Wajasiriamali hawa watapata ushauri maalum, rasilimali, na mtandao wa ushirikiano ili kuongeza athari zao na kuunda suluhisho endelevu kwa jamii za vijijini na mijini.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Larry Ayo, Mkurugenzi wa Biashara wa SmartLab, alisisitiza umuhimu wa mpango huu akisema:

“Ushirikiano wetu na EIT Climate-KIC unawawezesha wajasiriamali wa Kitanzania kupata zana za kuunda suluhisho endelevu la hali ya hewa. Ubunifu huu unakabiliana na changamoto muhimu za mabadiliko ya hali ya hewa huku ukiinua maisha ya jamii zinazohitaji msaada zaidi.”

Ufunguzi wa mpango huu ulifuatiwa na hotuba ya mgeni rasmi, Gerald David, Meneja mkuu Programu ya Global Resilience Partnership, ambaye alisema:

“Programu ya Adaptation and Resilience ClimAccelerator inaonyesha nguvu ya ushirikiano katika kushughulikia athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Programu kama hizi zinasaidia wabunifu wa ndani ya nchi kukabiliana na changamoto za kimataifa.”

Wakati hafla hiyo ikiendelea, baadhi ya wajasiriamali walipata nafasi ya kuonyesha kazi zao zinazoleta suluhisho katika sekta za kilimo na mifugo, usimamizi wa maji, misitu na matumizi ya ardhi, maeneo ya pwani, na makazi ya watu.

Hafla hiyo ilifungwa na hotuba ya shukrani kutoka kwa Edwin Bruno, Mkurugenzi Mtendaji wa Smart Africa Group. Edwin alisisitiza juhudi za pamoja za ushirikiano huu akieleza:

“Uzinduzi wa leo unaonyesha dhamira za dhati za washirika wote walioshiriki. Tunawashukuru  EIT Climate-KIC na Irish Aid kwa kutuamini na kutuunga mkono tunapojenga mustakabali endelevu kwa Tanzania.”

Programu hii ni sehemu ya Adaptation Innovation Cluster, mpango unaoongozwa na EIT Climate-KIC na kufadhiliwa na Irish Aid. Tangu 2019, EIT Climate-KIC imesaidia zaidi ya wabunifu 300 wa Kitanzania kupitia programu mbalimbali.

Awamu inayofuata ya mpango huu itaanza mapema 2025, ikilenga kusaidia wajasiriamali waliochaguliwa kukabiliana na changamoto za hali ya hewa na kuimarisha uthabiti katika jamii za vijijini.

Leave a Comment