×

Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili – 13

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Ghafla nilimwona ananikumbatia halafu akanielekeza kulala kitandani, nikaelekea hapo polepole huku mapigo ya moyo yakinienda kwa kasi ya ajabu.

“Shemeji Tiaki,” niliita.

“Naam.”“Unataka kufanya nini?”

ENDELEA SASA…

Nadhani nimefika hatua mbaya ya kuzidiwa. Jema linaweza kuwa baya. Lakini naomba langu liwe jema kwako na moyo wako.”

“Maongezi ni muhimu sana lakini,” nilimwambia Tiaki huku nikiwa nimelala kitandani.

“Ni kweli lakini nataka kukupa msimamo wangu kwamba, sitaweza kuoa mwanamke mwingine zaidi yako. Nimekuangalia tabia zako zote. Nimebaini unafaa kuwa mwenzangu,” Tiaki aliniambia kwa sauti ya upole na unyonge kiasi kwamba moyoni niliamini Tiaki hakuwa jini kutokana na alivyokuwa akizungumza na mimi.

“Tiaki ni kweli unanihakikishia kwamba unataka kunioa?”

“Kwa asilimia mia moja mama Kisu.”

“Mh! Mimi siamini mbona. Unajua kutoka kwenye ndoa na kuingia kwenye ndoa kunatakiwa uamuzi mgumu sana lakini siyo juu juu tu kama unavyotaka kufikiria wewe,” nilimwambia.

“Unataka kuamini kwa mimi kutumia njia gani? Maana kama unakumbuka vizuri niliwahi kukwambia kuwa, ukimaliza maombolezo niambie ili nianze kupitia hatua za kifamilia kuhusu wewe na mimi, nadhani sijui ndiyo ulishindwa kufanya hivyo kwa kuamini natania au vipi?”

Nilimwangalia Tiaki alivyokuwa akiongea mpaka nikajilaumu kwa kujiuliza ni kwa nini napoteza bahati yangu hivihivi?

“Nisamehe sana Tiaki. Sikuwa na nia hiyo lakini. Ila sasa naweza kusema yatatimia. Lakini itakuaje kuhusu makazi? Maana mimi mwenyewe nawaza namna ya kuondoka hapa?”

“Mama Kisu, mimi mwenyewe nilitaka kukwambia kitambo tu kwamba, kwa nini hapa usihame? Maana ninavyojua mimi, mmoja wa wanandoa akitangulia, si rahisi kwa aliyebaki kuendelea kudumu katika maisha yaleyale,” aliniambia Tiaki akiniangalia kwa karibu sana. Hapo tulikuwa bado chumbani kitandani tena!

“Niko tayari kuhama naangalia nihamie wapi maana hapa kodi sitaweza,” nilimwambia.

“Mimi nataka uhamie kwangu, lakini baada ya muda tukiwa tumeshafunga ndoa tutamalizia nyumba iliyopo Kibamba na kuhamia.”

Niliinuka kitandani, nikakaa. Nikamwangalia sana Tiaki nikimshangaa.

“Mbona umeshtuka sana mama Kisu?” aliniuliza.

“Kwani unajenga Kibamba?”

“Ndiyo, nyumba ipo kwenye rinta.”

“Kibamba gani?” nilimuuliza na kumkazia macho ili kuona kama atasema Kibamba gani.

“Kibamba CCM.”

“Tiaki please! Niambie ukweli kama wewe ni mume wangu baba Kisu! Please! Haiwezekani uwe na mambo kama yake au yetu. Hata sisi tunajenga Kibamba CCM, ujenzi umefikia kwenye rinta. Inakuaje iwe hivyo kwa karibu kila kitu?”

“Mama Kisu, sasa mimi niwe baba Kisu halafu nitake kukuoa tena jamani? Si ina maana ni mke wangu tayari!”

“Hapana Tiaki, wewe ni baba Kisu kabisa ila umegeuzwa na wabaya waliokuua na umekuwa hivyo sasa lakini wewe ni baba Kisu mume wangu.”

“Mh! Mama Kisu unakosea sana. Unatumia vigezo dhaifu sana. Mumeo alikuwa rafiki yangu mkuu. Ni hilo tu basi, mimi sijafanya na wala sijawahi kuwa baba Kisu aliyekufa na kubadilishwa.”

“Oke, niambie, wewe ulinunua hicho kiwanja kwa shilingi ngapi na nani alikuuzia ili nijue kuwa kweli wewe si baba Kisu kutokana na kile ulichokisema?” nilimuuliza, nikamwona anaangalia chini. Nikahisi amejua nimemkamata tayari.

“Nilinunua kwa shilingi milioni kumi, aliniuzia mzee mmoja lakini Mungu amuweke mahali pema peponi, alishafariki dunia.”

Nilimsukuma kwa nguvu Tiaki, akaanguka chini, nikatoka mbio kukimbilia sebuleni. Nilishika mlango mkubwa ili nitoke nje kabisa lakini Tiaki akawa ameshafika na kunishika mkono.

“Mama Kisu, una nini kwani? Mbona mimi kama sikuelewi? Mara unakuwa sawa, mara unakuwa kama una mawengemawenge!”

“Noo! Wewe baba Kisu ni kwa nini unaamua kunitesa hivi. Kama uliuawa na watu na unajua kwamba umekuwa roho nyingine niambie tu kuliko hivi unavyonifanyia. Unaniambia unajenga Kibamba wakati unajua kile kiwanja ni chetu sote, una maana gani sasa?” nilisema huku nikiangua kilio nikiwa nimeegemea mlango.

“Khaa! Mama Kisu, mimi siyo baba Kisu, mbona huamini lakini shemeji? Una nini kwani! Acha kunifikiria vibaya,” alisema Tiaki huku akiwa amenishika mkono na kunirudisha chumbani.

Nilikubali nikamfuata nyumanyuma hadi chumbani, akakaa kitandani na mimi nikakaa pia pembeni yake huku nikiendelea kulia na kumtafakari. Niliamini kifo changu kiko jirani sana kuliko wakati mwingine wowote ule.

“Mama Kisu?”

“Abee,” niliitika huku nikiwa nimeuficha uso wangu kwa sehemu ya juu ya kiganja na nilijua anachotaka kusema ni kukiri kwamba kweli yeye ni mume wangu, marehemu baba Kisu.

Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili wiki ijayo.

Leave a Comment