
Tukio la kusikitisha limetokea katika Mtaa wa Mkudi, Manispaa ya Ilemela, ambapo kijana aitwaye Adam Kailanga (30) amemuua mpenzi wake, Benadeta Silvester (21), ambaye anadaiwa kuwa mwanafunzi wa Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari Korogwe, kisha naye kujiua kwa kujinyonga kwa kutumia mtandio.
Kwa mujibu wa mashuhuda, wawili hao walikuwa na ugomvi mkali kabla ya tukio, ambapo Adam alimshutumu Benadeta kwa kuwa na mahusiano na wanaume wengine. Ingawa majirani walijaribu kuingilia kati na kuwasuluhisha, baadaye waligundua wawili hao wamepoteza maisha baada ya kufungua mlango wa nyumba waliyokuwa wakiishi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna Wilbroad Mutafungwa, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea, ikiwemo kuwasiliana na shule aliyokuwa akisoma marehemu Benadeta.
Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure.