×

Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Afunga Mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Viwanda vya Kijeshi

Dar es Salaam 26 Februari 2025: Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salum Othman, leo amefunga rasmi Mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Viwanda vya Kijeshi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao umefanyika jijini Dar es Salaam kwa muda wa siku mbili.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Luteni Jenerali Salum Othman amesema lengo la wakuu hao kukutana ni kuwasilisha, kujadili, kushirikishana uzoefu wa kina na kutafakari masuala yanayohusu maendeleo ya sekta ya Viwanda vya Kijeshi. Ameendelea kusema kuwa wakuu hao wameonesha kiwango cha juu cha kujitolea na kufanyakazi kwa bidii ili kuwezesha maendeleo makubwa katika sekta ya viwanda vya kijeshi katika nchi hizo ambapo alisema;

“Majeshi yetu yanahitaji vifaa mbalimbali ili kutekeleza kwa ufanisi majukumu tuliyopewa na serikali zetu.

“Ili kupata vifaa hivyo, ambavyo mara nyingi ni ghali sana, kwa kawaida huwa tunavitafuta kwenye masoko ya kimataifa kwa njia ya msaada au ununuzi.

“Hata hivyo mara kwa mara tunakumbana na masharti yanayowekwa na wauzaji huko tunaponunua vifaa hivyo.

“Vikwazo hivyo vinavyowekwa mara nyingi huathiri uhuru wetu wa kuvitumia.

“Kwa hiyo, ninafurahishwa na juhudi za nchi zetu kuelekea kujinasua na hali hiyo.

“Licha ya kuwa na utaifa tofauti, mmeunganishwa na dhamira moja ya kufanikisha maendeleo ya viwanda vya kijeshi kwa pamoja.

Kwa hakika, huu ni uthibitisho wa kujitoa kwetu na nia yetu ya dhati katika kuimarisha ushirikiano wa ulinzi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, jambo ambalo linastahili kupongezwa”. Amesema Luteni Jenerali, Salum Othman.

Ameendelea kusema kuwa maendeleo katika sekta ya viwanda ni kiashiria kikuu cha kiwango cha maendeleo ya nchi yoyote duniani.

Nchi zinazoitwa zilizoendelea ni zile ambazo zimepiga hatua kubwa katika viwanda.

Hivyo basi, kama nchi zetu zinataka kuendelea, hatuna budi kufanya yale ambayo tayari mmekuwa mkifanya.

“Maonyesho ya Viwanda vya Ulinzi yaliyoandaliwa na Viwanda vya Ulinzi vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yameonyesha maendeleo makubwa tuliyopiga katika kujenga uwezo wetu wa kujilinda.

Hili ni dhihirisho la juhudi zetu za pamoja za kukuza kujitegemea katika ukanda wetu na kuuza bidhaa na malighafi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pamoja na mafanikio haya, napenda kuwasihi msitosheke na mafanikio haya bali mjitahidi zaidi ili kufanikisha uhuru mkubwa wa viwanda vyetu na ushirikiano wa kina zaidi.

“Nikitambua kuwa hitimisho la mkutano huu ni mwanzo wa mkutano mwingine, nawahimiza nyote kudumisha moyo wa majadiliano ya wazi na wa ukweli ambao umeonyesha katika kongamano hili.

“Ni kupitia mtazamo huu wa ushirikiano ndipo tutaweza kukabiliana na changamoto tunazokumbana nazo na kutumia fursa zilizopo kwa manufaa yetu.

“Kwa kumalizia, ningependa kutoa shukrani za dhati kwa kila mmoja wenu kwa ushiriki wenu hai na michango yenu yenye thamani.

“Uwepo wenu hapa ni ishara ya imani na matumaini ambayo nchi zenu zimewawekea.

Ninaamini kwamba roho hii ya mshikamano itaendelea kudhihirika tunapoendelea kuimarisha na kupanua ushirikiano. Alimaliza kusema Luteni Jenerali, Salum Othman.

Nae Mkuu wa Shirika la Mzinga, Brigedia Jenerali, Seif Hamisi baada ya mkutano huo kufungwa amesema kuwa huo ni mkutano wa kawaida wa mwaka ambao huwa unafanyika kila mwaka na mwaka ujao wanatarajia kufanyia katika nchi ya Rwanda. HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS NA NEEMA ADRIAN /GPL