×

Dkt. Gwajima Apongeza Jeshi La Polisi Kuzuia Vitendo Vya Ukatili

Dkt Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Jeshi la Polisi kupitia Mtandao wa Askari Polisi Wanawake (TPF-NET) na Dawati la Jinsia na Watoto nchini limepongezwa kwa kufanya kazi vizuri kuhakikisha matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto yamekomeshwa kwenye jamii.

Hayo yamebainishwa Machi 02, 2025 Wilayani Bukombe na Dkt Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika Kongamano la kuelekea siku ya Wanawake Duniani Kanda ya Ziwa lenye kauli mbiu ya “Wanawake na Wasichana 2025; Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji” ambapo Maafisa, Wakaguzi na Askari wa Jeshi la Polisi wameshiriki kikamilifu.

“Ukiona mimi ninatamba huko, ujue ni Mtandao wa Polisi Wanawake na Dawati la Jinsia na Watoto”. Amesema Dkt. Gwajima.

Kadhalika, Dkt. Gwajima ameeleza mafanikio ya wanawake katika uongozi ambapo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameendelea kuwateua wanawake katika nafasi mbalimbali za ungozi na wameonesha uwezo mkubwa wa kuongoza.

Vile vile, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Sarafina Chamlonde akitoa taarifa fupi katika banda la Polisi Wanawake kwenye Kongamano hilo, ameeleza nafasi ya Mtandao wa Askari Polisi Wanawake katika Jeshi la Polisi na jamii kwa ujumla kuhakikisha Wasichana na Wanawake wanalindwa dhidi ya ukatili wa kijinsia ili kutimiza ndoto na malengo yao.