CATARINA amenusurika kifo kwa kuokolewa na vijana wawili ambao wameamua kumsaidia ili kuhakikisha Motown anakamatwa na kufikichwa mbele ya sheria, wamemficha ndani ya nyumba yao na wao kwenda kutoa taarifa kwenye ofisi za FBI ambako wanatoa maelezo yote na FBI wanaongozana nao kwenda huko.
Gari linaendeshwa na hatimaye wanafika lakini cha kushangaza wanapoingia ndani ya nyumba, hawamkuti Catarina badala yake wanaona damu nyingi zikiwa zimetapakaa sakafuni.
Wanaingiwa na hofu huku wakiamini kwamba pengine Jackson Motown akishirikiana na kundi lake walimteka Catarina na kumuua.
Wakijaribu kujitetea afisa mmoja wa FBI anaamuru wazungushe mikono yao nyuma na pingu zinaingia, wanaingizwa kwenye gari na safari kuelekea kwenye ofisi za FBI inaanza.
Je, nini kitaendelea?
SONGA NAYO…
DEREVA aliyekuwa kwenye usukani wa gari la FBI, aina ya Ford 220, toleo jipya alikuwa ni Sajenti John Pearson, akilini na moyoni mwake akiwa amejawa na hasira nyingi sababu ya kudanganywa na kuachishwa kazi zake ofisini kisha kuletwa mahali alikotarajia kumwona Catarina lakini akaishia kumkosa, kabla hajakata kona kuingia kulia, alitupa jicho kwenye kioo cha kuongozea gari cha upande wa kulia ambacho kwa Kiingereza huitwa Side Mirror na kuangalia nyuma.
“A woman is running after our car!” (Kuna mwanamke analikimbiza gari letu!)
“Really?” (Kweli?)
“Yeah! Look over your shoulder you will see her!” (Ndiyo! Ngeuka nyuma utamwona!) John Pearson akasisitiza akikanyaga breki na kupunguza mwendo, watu waliokuwa nyuma ya gari wakiwemo vijana wawili waliopigwa pingu mikononi waligeuka na kupiga kelele;
“She is the one!” (ni yeye!)
“Who?” (Nani?)
“Catarina!”
“Reverse please!” (Rudisha gari kinyumenyume tafadhali!) askari mmoja alimwamuru dereva naye akafanya hivyo, mlio wa ‘Ndii! Ndii! Ndiii!’ ukasikika wakati gari likirudi kinyumenyume kwa kasi mpaka likamfikia mwanamke aliyekuwa akija mbio.
“Where were you Catarina?” (Ulikuwa wapi Catarina?) mmoja wa vijana hao alimuuliza gari liliposimama.
“I went to the nearby grocery store to buy some stuff because few minutes after you left, I notice a profuse menstrual bleeding, spent your ten dollars bill which was on the table to buy this, I can prevent the blood from dripping on the floor!” (Nilikwenda kwenye kiduka kidogo cha jirani kununua vitu kwa sababu muda mfupi baada ya ninyi kuondoka, niligundua damu nyingi ya hedhi inanitoka, nimetumia dola kumi iliyokuwa juu ya meza kununua hizi, ili nizuie damu kudondoka sakafuni!)
“Oh my God! We thought you have been captured by Jackson Motown’s gang!” (Oh Mungu wangu! Tulifikiri umetekwa na kundi la Jackson Motown!)
“No! I am very fine, why are you handcuffed?” (Hapana! Niko vizuri, mbona mmepigwa pingu?)
“They thought we are lying!” (Walifikiri tunadanganya!)
“On?” (Juu ya?)
“That you are alive!” (Kwamba uko hai!)
“I am alive and you are the ones who saved my life!” (Niko hai na ninyi ndiyo mliokoa maisha yangu!)
Maofisa wa FBI wakiwa wamepigwa na butwaa waliwafungulia vijana wale pingu mikononi kisha kumwomba Catarina aingie ndani ya gari, akafanya hivyo na wakaondoka naye kwa kasi kuelekea ofisi za FBI New York ambako aliingizwa kwenye chumba maalum cha kufanyiwa mahojiano akiwa na vijana wale.
Katika mahojiano yao Catarina alielezea mkasa mzima wa kubakwa na tajiri Jackson Motown mpaka kupoteza fahamu na baadaye kutaka kuzikwa ndani ya Uwanja wa Ndege wa JF Kennedy, lakini vijana aliokuwa nao hapo ndiyo waliomwokoa, maelezo yake hayakutofautiana kabisa na yaliyokuwa yametolewa na waokoaji wake kabla hajapatikana, ilikuwa ni habari ya kusikitisha na ya kushangaza kwa mtu kama Jackson Motown kutenda jambo baya kama hilo katika jamii.
“He is a bad guy, he has to be arrested!” (Ni mtu mbaya, lazima akamatwe!) alisema mmoja wa maofisa hao.
Uamuzi walioufikia ni kupandisha ofisini kwa bosi wao na kumpa taarifa juu ya tukio zima, hata yeye alisikitika kupita kiasi, ikaamriwa Jackson Motown akamatwe mara moja na Catarina apewe ulinzi maalum, sababu mbele ya safari angehitajika kutoa ushahidi mahakamani wakati wa kesi ya Jackson Motown, mtu mwenye nguvu na ushawishi ikiendelea.
“Send a team to Miami for Jackson Motown’s arrest!” (Tumeni kikosi kwenda Miami kumkamata Jackson Motown!) Bosi aliamuru.
Catarina alichukuliwa na kupelekwa Hoteli ya Hilton New York ambako alichukuliwa chumba na kupewa ulinzi maalum, vijana waliomwokoa wakaruhusiwa kurejea nyumbani kwao wakiwa wameelezwa kwamba mara wakihitajika wangepigiwa simu mara moja.
Hilo ndilo kosa walilolifanya FBI kwani vijana hao na wenzao wote siku mbili baadaye walikutwa ndani ya nyumba zao wamekufa wakiwa wamejidunga sindano kwenye mshipa wa damu. Siku chache tena baadaye Mario Pizaro naye alikufa katika mazingira ya kutatanisha, kifo chake kikiacha maswali mengi vichwani mwa watu.
***
Maofisa wa FBI walipofika Miami nyumbani kwa Motown hawakumkuta, si yeye tu bali pia wasaidizi wake, hapakuwa na mtu mwenye uwezo wa kueleza ni wapi hasa alikokuwa. Baadaye walipata nafasi ya kukutana na mfanyakazi wa bustanini ambaye baada ya kujitambulisha alikubali kuongea nao ingawa kwa masharti ya kutotajwa mahali popote.
“Mara ya mwisho ni siku chache zilizopita aliporejea kutoka kwenye mazishi ya Mario Pizaro, aliondoka hapa na vijana wake usiku, hawakurudi tena mpaka leo, sijui walikokwenda!”
“Una namba yake ya simu?”
“Sina lakini ninayo ya mlinzi wake Dragon!”
“Unaweza kumpigia?”
“Halafu nimuulize nini?”
“Kama yuko na bosi?”
“Hapana, atahisi kwamba mimi nimeshirikiana na ninyi kama ikitokea akapata matatizo, yule ni mtu hatari, anaweza hata kuniua!”
“Tupe hiyo namba, sisi tutafahamu mahali alipo!”
“Sawa,” alijibu kijana yule na kuwatajia namba ya Dragon, wakamuaga na kuondoka.
Kitu cha kwanza walichokifanya baada ya kurejea New York ni kwenda hotelini kwa Catarina, walimkuta akilia kwa uchungu mno kufuatia habari kwamba vijana wote waliomwokoa walikuwa wamekufa, alisema bila kupindisha maneno kwamba aliyefanya hivyo hakuwa mtu mwingine bali Jackson Motown akijaribu kuficha ubaya wake.
“Jamani nilindeni, hata mimi ataniua na nina wasiwasi sana atakuwa amemuua Kevin!”
“Tunafuatilia.”
“Jitahidini jamani!”
“Usiwe na wasiwasi, tumepata namba ya mlinzi wake Dragon, tukifika ofisini na kuiweka kwenye mitambo yetu itatuonyesha mahali alipo Dragon, bila shaka hata Jackson Motown atakuwa hapo!”
“Inawezekana!”
“Pumzika tutawasiliana na wewe baadaye!” walijibu na kuondoka, maongezi yao yote yalifanyika katika Lugha ya Kiingereza.
Maofisa wa FBI wakaondoka hadi ofisini kwao na kutoa taarifa kwa bosi, kisha kuingiza namba ya Dragon kwenye mtambo wao uitwao GPS Tracer, ambao husaidia kuonyesha mahali namba ya simu inapotumika, haikuchukua hata dakika kumi ikaonyesha kuwa Dragon alikuwa eneo la mashambani, kilometa mia moja na themanini kutoka Miami, liitwalo Opa-Locka.
“Sijui anafanya nini huko?”
“Lazima twende tukajue, kuna uwezekano mkubwa kabisa wako hapo na Jackson Motown wamejificha.
Je, nini kitaendelea? FBI watafanikiwa kumpata Jackson Motown? Fuatilia kesho katika Gazeti la Championi Jumamosi.