×

Waziri Mkuu Majaliwa awataka wavuvi Buchosha kuunda vikundi wasaidiwe

Waziri Mkuu Kasim Majaliwa amewataka vijana wa Jimbo la Buchosha ambao ni wavuvi kuunda vikundi ili waweze kusaidiwa kwa zana za uvuvi kwa urahisi.

Ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Buchosa na akasisitiza kwamba nia ya serikali kuhakikisha wavuvi waendelee na uvuvi kwani uvuvi ni utajiri, uvuvi ni maisha na akawataka wavuvi kufanya kazi kwa bidii na kwa amani ili kujiletea maendeleo.

Amewaambia vijana Buchosa kuwa wakiwa kwenye vikundi inakuwa rahisi kuaminika na kusaidiwa. Aidha Waziri Mkuu Majaliwa amesema ana tarifa kwamba ziwa Victoria wilaya ya Sengerema limevamiwa na magugu maji yaliyoenea kama kilomita 500 na serikali imeanza kuyashughulikia. Amesema kuna meli maalum zitafanya kazi ya kuondoa magugumaji hayo.

“Serikali imeagiza meli kubwa mbili zenye mashine ya kushughulikia magugu maji na sasa tuna meli moja ndogo ambayo inasagasaga magugumaji na kuyatupa pwani ya ziwa. Magugumaji hayo ni mengi kiasi kwamba mtu anaweza kusimama juu ukadhani yupo nchi kavu.

Ni hatari sana, haya tutapambana nayo na popote mtakapoyaona toweni taarifa ili yashughulikiwe,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akizungumzia Chuo Cha Ufundi (VETA) Waziri Mkuu Majaliwa amesema Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo na bunge wa Sengerema, Tabasamu ni wabunge wanaoshirikiana sana na walikubaliana kijengwe chuo cha VETA Buchosa na kimejengwa.

“Sijawahi kuona wabunge wanaoshirikiana kama wabunge hawa, Mheshimiwa Shigongo na Mheshimiwa Tabasamu, walikubaliana wawe na chuo cha VETA na sasa chuo kipo tayari Buchosa vijana nendeni mkasomee kisha mrudi nyumbani mkafanye kile mlichosomea,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Stori na Elvan Stambuli GPL.