×

Madeleka Asema Akigombea Ubunge Tume Huru Ya Uchaguzi Itamtangaza Kuwa Mshindi

Wakili wa Kujitegemea Peter Madeleka amesema endapo atagombea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu (2025) basi ana uhakika usiokuwa na shaka kwamba Tume Huru ya Uchaguzi Nchini (INEC) itamtangaza kuwa mshindi katika kinyang’anyiro hicho

Wakili Madeleka amezungumza hayo leo, Jumanne Mei 20.2025 kwenye ofisi za makao makuu ya Chama cha ACT Wazalendo zilizopo Magomeni, jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara Isihaka Mchinjita kutangaza kuwa Wakili huyo maarufu sasa amejiunga na hama hicho

“Hakuna mtendaji yoyote wa Tume ya Uchaguzi ambaye hawezi kunitangaza, nina majimbo kama matano (5) hivi ambayo nikienda kugombea kote natangazwa, kote nitatangazwa na napenda nikualike kabisa ili ufuatilie kampeni zangu ujuwe na hizo mbinu za kampeni, fuatilia kampeni zangu, mbinu nitakazokuwa natumia kwanza kuwaonyesha CCM kwamba mimi nashinda huu uchaguzi” -Wakili Madeleka

Akijibu hoja ya kudai kwamba yeye anatumika na ‘dola’ kwakuwa amewahi kuwa mtumishi wa umma (Afisa wa Jeshi la Polisi) Wakili Madeleka amesema madai hayo hayana msingi wowote bali ni ‘propaganda’ na kwamba katika historia ya Tanzania kumeshuhudiwa maafisa kadhaa waliotoka kwenye vyombo vya Ulinzi na Usalama iwe kwa kuacha kazi au kustaafu wakijiunga na vyama vya siasa tofauti nchini ikiwemo CCM, CUF na CHADEMA

“Muongozu wa Katiba ya Tanzania uko wazi, kuwa mtumishi wa umma ukitaka kuingia kwenye siasa ni lazima uache kazi, sasa mimi sio mtumishi wa kwanza kuwa afisa wa vyombo vya ulinzi na usalama kuacha kazi hiyo na kufanya siasa, na utumishi wangu katika nchi hii kila mtu anajuwa namna gani umekoma na ndio maana niko mtaani naendelea kufanya shughuli zangu” -Wakili Madeleka.