×

Fred Lowassa Amuenzi Dkt. Mengi, Amtambua Bilionea Mulokozi

Mbunge wa Jimbo la Monduli, Fred Lowassa, amewataka Watanzania kumuenzi kwa vitendo hayati Dkt. Reginald Mengi kwa kuwawezesha watu wenye ulemavu kijamii na kiuchumi. Aidha, amemtaka mfanyabiashara bilionea David Mulokozi kuendeleza kazi nzuri zilizofanywa na Dkt. Mengi, hasa katika kusaidia makundi maalumu kupitia misaada mbalimbali kama ambavyo amekuwa akifanya mara kwa mara.

Lowassa alitoa kauli hiyo katika hafla ya kukabidhi misaada kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo viti mwendo, vifaa vya shule na majiko ya gesi. Misaada hiyo imetolewa na shirika lisilo la kiserikali la Sywso, kwa ufadhili wa Taasisi ya Mati foundation, iliyoanzishwa na bilionea Mulokozi kwa lengo la kusaidia jamii.

Mbunge huyo alimpongeza Mulokozi kwa kuwa mfano bora wa kuigwa, kutokana na kutumia sehemu ya faida ya biashara zake kusaidia Watanzania, hasa walioko kwenye mazingira magumu.

Kwa upande wake, Afisa Miradi wa Mati Foundation, Izack Piganio, alisema taasisi hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa watu wenye uhitaji, ikiwa ni pamoja na viti mwendo kwa watu wenye ulemavu, pamoja na misaada ya kibinadamu katika maeneo mbalimbali nchini.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Sywso, Omega Mlay, alisema wataendelea kuwasaidia watoto wenye ulemavu katika Kata ya Makuyuni kupitia mradi wao mpya wa “Mwendo wa Matumaini” uliozinduliwa rasmi leo.