
Dodoma, 19 Juni 2025: Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani, bado ipo katika mchakato wa kupitia maelekezo ya sheria kuhusiana na Sekta ya Ulinzi Binafsi Nchini, kutokana na ukweli kwamba Makampuni ya Ulinzi yamekuwa yakihudumu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo ya binafsi na Serikalini kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Maduhu Isack Kazi aliyemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu wa Kazi wa Chama cha Sekta Binafsi ya Ulinzi Nchini.
Amesema, “wamekuwa wakifanya vizuri lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kushindwa kuwalipa wafanyakazi wao kwa wakati, hizi ni moja ya changamoto ambazo zinahitajiwa kufanyiwa kazi.”

Dkt. Kazi ameongeza kuwa, mchakato huo pia unataka kwa ushirikiano kulishughulikia suala la ucheleweshaji wa malipo na kuhakikisha Wafanyakazi wa Kampuni hizo wanapata haki zao stahiki, ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Awali, Mwenyekiti TSIA-Taifa, Felix Kagisa alisema kuna ombwe kubwa la kisheria hali inayofanya watumie sheria ya kiraia inayowaruhusu kugoma wawapo kazini jambo ambalo linapaswa kushughulikiwa kutokana na unyeti wake.

“Kuna vurugu ya kutoelewana katika sekta hii muhimu, hebu angalia kama wanaruhusiwa kugoma kwa sheria iliyopo na wana silaha hawa watu unadhani itakuwaje? Ni kweli wanapitia magumu lakini ipo haja ya kuboresha mapungufu yaliyopo lakini na sheria zibadilike,” alisema Kagisa.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Polisi, DCP. Henry Mwaibambe ambaye amezungumza kwa Niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma, ACP Galus Hyera amekiri uwepo wa changamoto zilizoainishwa na wazungumzaji wa awali, huku akisisitiza kuwa hilo halitafanya wao kushindwa kusimamia sheria zilizopo.