
KAMPUNI ya kutengeneza bia nchini, Tanzania Breweries (TBL) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini wamezindua alama maalum za waendesha pikipiki (bodaboda) kwenye mataa ya kuongozea vyombo vya moto lengo likiwa kupunguza ajali za bodaboda nchini.
Akizungumza kwenye uzinduzi Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Wilbroad Mutafungwa aliyekuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi amesema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu kulikuwa na ajali za pikipiki 296 zilizosababisha vifo vya watu 211 na majeruhi 212.

Kamanda Mutafungwa amesema hayo Oktoba 15, 2022 wakati uzinduzi wa maeneo salama ya kusubiria (Buffer Zone) kwa waendesha pikipiki hasa wanapofika katika makutano ya barabara yanayoongozwa na alama, michoro na taa za kuongozea watumiahi wa barabara,magari, pikipiki na watembea kwa miguua.

“Tunaishukuru Serikali kupitia TANROADS kuona umuhimu wa kuwa na maeneo salama kwa kundi hili la watumiaji wa barabara .Niwashukuru wadau wetu wa usalama barabarani TBL wa kuona umuhimu wa kushiriki kwa ufadhili wa hali na mali.

“Katika utoaji elimu ya usalama barabarani na kutumia sehemu ya faida yao kwa manufaa ya watumiaji wa barabara hasa waendesha pikipiki,”amesema Kamanda Mutafungwa na kuongeza katika Wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkoani Arusha TBL kushirikiana na Tanroad na Polisi walizindua mpango huo kwa watumiaji wa barabara hasa waendesha bodaboda. Ameongeza na leo katika ushirika ule ule wanakwenda kuzindua mpango huo jijini Dar es Salaam na kutoa ombi kwa mikoa mingine wafanye hivyo kwa manufaa na usalama wa watumiaji wa barabara.
“Uzinduzi wa maeneo ya Buffer Zone kwa waendesha pikipiki hasa wanapofika makutano ya barabara yanayoongozwa na alama, michoro na taa za kuongozea watumiaji wa bararabara ni muhimu sana katika dhana nzima ya usalama barabarani kwa kulinda maisha ya watu na mali zao watumiapo barabara.”

Aidha amesema wamekuwa wakishuhudia ajali nyingi zikitokea katika maeneo hayo hasa kwa kuwa madereva wa pikipiki wanakosa elimu na maarifa ya kutosha kuepusha ajali za barabarani ama kwasababu ya kutojua au kupuuzia na kudharau kwa kutotii sheria za barabarani.
Kamanda Mutafungwa amesema katika makundi ya watumiaji wa barabara , waendesha pikipiki maarufu bodaboda ni kundi kubwa ambalo linashiriki kutoa huduma ya usafiri kwa watu wengi , hivyo linapaswa kuwa na elimu ya kutosha kuhusu matumizi sahihi ya alama za barabara.
Ameongeza kwa Jeshi la Polisi, kikosi cha Usalama Barabara litaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kundi hilo kubwa linafikiwa kwa elimu ya sheria za usalama barabarani kwa lengo la kuokoa maisha ya watu na mali zao. Aidha ametoa rai kwa waendesha bodaboda kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu wa kijinai kwani baadhi yao wanapojihusisha wanaharibu sifa ya biashara ya kusafirisha abiria kwa bodaboda.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TBL, Jose Moran alisema, “Kila maisha yana thamani isiyopimika. Kila hasara inawakilisha uwezo ambao haujatimizwa. Inasikitisha sana kupoteza watu wengi huku ukizingatia kuwa mara nyingi ajali hizi zinaweza kuzuilika.”
Alama za kanda za bafa (Buffer zones) ni kuongoza kwenye makutano ya barabara yenye shughuli nyingi, ambazo zinadhibitiwa na taa za trafiki, ambazo zitatenganisha pikipiki na magari mengine. Haya yanajiri baada ya uchanganuzi unaoonyesha ajali nyingi zinazotokea kwenye makutano kutokana na mwingiliano wa fujo wa pikipiki na magari. Kama uthibitisho wa dhana, maeneo ya buffer yaliyoanzishwa nchini Brazili yalipunguza ajali zinazohusisha pikipiki kwa 25% katika mwaka mmoja. Alisema Moran
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Ilala amesema leo wamekuwa kwenye zoezi la kuweka alama za barabarani hasa kwa waendesha bodaboda ambao ni usafiiri muhimu katika jiji la Dar es Salaam. “Mimi kama msimamizi wa shughuli za Serikali jambo hili ni nzuri ambalo linafanywa na wenzetu wa Polisi pamoja na TBL lakini likishirikisha waendesha bodaboda na lengo kubwa ni kuhakikisha kunakuwa na usalama kwa watumiaji wote wa barabara ni muhimu kwa kila mtumiaji wa barabara kuheshimu alama zilizowekwa.
“Kwasababu lengo kubwa ni kuhakikisha kila mtumiaji wa barabara anakuwa salama, hapa mjini tumekuwa tukipokea changamoto nyingi hasa matukio ya ajali ambayo yamekuwa yakipunguza nguvu kazi ya Taifa kwa vijana , abiria kupata ulemavu. Hivyo tunapongeza jitihada hizi,”amesema Ludigija. Ameongeza matarajio yake ni kuona alama hizo za waendesha pikipiki zinakuwa katika barabara zote za TANROADS, TARURA kwa ajili ya kuokoa maisha ya watanzania na mwito wake kwa waendesha bodaboda kuheshimu alama za barabara kwasababu ya usalama wa maisha yao na abiria.