×

Lissu Afikishwa Mahakama Kuu Kupinga Ushahidi wa Mashahidi wa Siri

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Antiphas Lissu, ameonekana leo Alhamisi Juni 26, 2025, ndani ya Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, kufuatilia shauri la Jinai Na. 14496/2025, dhidi ya Jamhuri.

Lissu anaiomba Mahakama hiyo Kuu iangazie upya na kutoa uamuzi kuhusu uhalali wa ushahidi wa mashahidi wa siri, ambao uliruhusiwa na hakimu anayeendesha kesi ya uchochezi inayomkabili katika Mahakama ya Mwanzo.

Katika hoja zake, Lissu kupitia mawakili wake, anapinga vikali hatua hiyo ya upande wa Jamhuri kuwasilisha mashahidi wa siri akisema inakiuka haki yake ya msingi ya kujitetea ipasavyo. CHADEMA, kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, imesema kuwa Lissu hakufahamu awali kuhusu uamuzi huo, na kwamba utaratibu huo unaweza kuathiri haki, uwazi na usawa wa mchakato mzima wa kesi.

“Tunaamini kuwa haki ya kujitetea ni nguzo kuu ya mfumo wowote wa sheria. Mashahidi wa siri wanaweza kuathiri uamuzi wa kesi kwa njia isiyo ya haki na isiyo ya uwazi,” CHADEMA imeeleza.

Kwa sasa, Mahakama Kuu inaendelea kusikiliza hoja za pande zote kabla ya kutoa maamuzi yatakayobainisha kama ushahidi huo utaendelea kutumika au la.