×

Mazungumzo Ya Kusitisha Vita Gaza Yagonga Mwamba

 

(Kushoto) Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel ; (Kati)Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani, Waziri Mkuu wa Qatar na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ; (Kulia) Ismail Haniyeh, Kiongozi wa Hamas

Duru ya kwanza ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya kusitisha mapigano kati ya Wapalestina na utawala wa Israel, yaliyofanyika nchini Qatar, yamemalizika bila mafanikio yoyote, kwa mujibu wa vyanzo viwili vya Palestina vinavyofahamu majadiliano hayo.

Kwa mujibu wa Iran Press, licha ya juhudi za kimataifa na duru nyingi za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, mivutano muhimu baina ya pande mbili hizo bado haijatatuliwa. Israel inapinga mapendekezo ya marekebisho yaliyowasilishwa na Hamas kabla ya kusainiwa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Vifusi vya majengo yaliyobomolewa baada ya mashambulizi ya anga ya Israel, Palestina (Gaza)

Mvutano huu unaendelea huku wanajeshi wa Israel wakiendelea kuwauwa kikatili Wapalestina katika Ukanda wa Gaza kila siku, na hivyo kuzidisha idadi ya watu waliouawa katika eneo hilo lililozingirwa.

Vyanzo vya Palestina vimeripoti kuwa, “Ujumbe wa Israel haujaidhinishwa vya kutosha kufikia makubaliano na Hamas.” Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema Wapatanishi wa Israel wamepewa maagizo ya wazi ya kufikia usitishaji wa mapigano kwa masharti ‘yanayokubalika’ kwa Israel.

Rais wa Marekani, Donald Trump

Haya yanajiri licha ya Rais wa Marekani, Donald Trump kudai hivi karibuni kuwa, “Kuna nafasi nzuri ya kufikia makubaliano na Hamas wiki hii. Nadhani tunakaribia makubaliano kuhusu Gaza.”