
Klabu ya Yanga SC leo imezindua rasmi kampeni maalum iitwayo ‘Tofali la Ubingwa’, ikiwa ni mpango wa kipekee wa kuhusisha mashabiki na wanachama moja kwa moja katika maendeleo ya timu, hususan kwenye eneo la usajili wa wachezaji wa kimataifa na wenye viwango vya juu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Msemaji wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe, amesema kuwa lengo la kampeni ni kuimarisha nguvu ya kifedha ya klabu kupitia michango ya hiari kutoka kwa mashabiki, ili kuwezesha usajili wa wachezaji bora watakaokwenda kuongeza ubora ndani ya kikosi kuelekea msimu mpya.
“Kupitia Tofali la Ubingwa, mashabiki wa Yanga sasa wana nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika mafanikio ya timu. Kila mchango wao ni tofali linalojenga msingi wa kikosi bora, chenye ushindani wa kimataifa,” alisema Kamwe.
Ameongeza kuwa kampeni hiyo inakuja katika wakati muafaka ambapo Yanga SC inajiandaa kushiriki michuano ya CAF Champions League msimu wa 2025/2026, na hivyo inahitaji kikosi imara kitakachoweza kuwika barani Afrika.
Kwa mujibu wa Kamwe, michango ya mashabiki itatumika moja kwa moja kwenye usajili wa wachezaji wapya, hivyo kuwapa nafasi wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kuwa sehemu ya maamuzi na mafanikio ya timu yao.