
JUZI Jumatano, Ndanda FC iliifunga Mwadui FC na kufufua matumaini ya kusalia kwenye Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.
Ushindi huo wa Ndanda wa mabao 3-0, uliwashangaza wengi kutokana na aina ya mabao yake ambayo mawili ya kwanza yaliingia ndani ya dakika tano za kwanza. Lingine likafungwa muda mchache kabla ya kwenda mapumziko.

Tunafahamu kwamba mchezo wa soka unakuwa na matokeo ya kushangaza ndiyo maana Ndanda iliweza kufunga mabao hayo ambayo tangu kuanza kwa msimu huu haijawahi kufunga kwa staili hiyo.
Ndanda hivi sasa inahitaji ushindi katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya Stand United ili ijihakikishie kubaki, wakati Majimaji nayo inahitaji ushindi mbele ya Simba, huku ikiomba Ndanda ipoteze, iweze kuepuka kushuka daraja.

Kwa sasa timu hizo mbili zinapigana vikumbo kukwepa mkasi wa kushuka daraja kwani baada ya Njombe Mji kushuka, imesalia nafasi moja ambayo kati ya Ndanda na Majimaji, mmoja atahusika. Ndanda ina pointi 26, Majimaji 24 na zote zimesaliwa na mechi moja watakazocheza nyumbani.
Katika kumalizia msimu ili kusiwe na dosari yoyote ile ya upangaji matokeo, ni wazi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likawa macho na suala hilo.
Hivi sasa vita ya ubingwa hakuna tena kutokana na Simba kuwa bingwa ikiwa na michezo mitatu mkononi, kilichosalia ni vita ya kushuka daraja ambayo imebaki kwa timu hizo mbili.
Kwa kuwa zote zinacheza nyumbani na kama inavyofahamika kwamba siku zote ukicheza nyumbani unakuwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri, basi timu iweze kupata matokeo hayo mazuri kwa uwezo wake na si kwa kutafuta nguvu ya mwingine.