
Klabu ya Simba Sports Club imekamilisha usajili wa mshambuliaji hatari raia wa Ghana, Jonathan Sowah, ambaye ametambulishwa rasmi kama mchezaji mpya wa Wekundu wa Msimbazi kwa mkataba wa miaka miwili, ambao utamuweka klabuni hadi Juni 2027.
Sowah (26), anajiunga na Simba SC akitokea klabu ya Singida Black Stars, ambapo katika msimu uliopita alionesha kiwango cha juu kwa kufunga mabao 15 kwenye mechi 15, akithibitisha uwezo wake mkubwa wa kumalizia nafasi akiwa mbele ya lango.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Simba SC, moja ya sababu kubwa iliyowavutia kumsajili mshambuliaji huyo ni uwezo wake wa “kubadilisha nafasi moja kuwa bao”, jambo ambalo linaendana na mahitaji ya kikosi cha kocha Abdelhak Benchikha kwa msimu ujao.
“Simba ni timu kubwa. Mara tu walivyonitafuta, haikunichukua muda kukubali. Ni ndoto ya kila mchezaji kupata nafasi kama hii,” amesema Sowah mara baada ya kusaini mkataba wake.
“Malengo ya klabu yanaendana na malengo yangu binafsi. Mimi ni mshambuliaji – kazi yangu ni kufunga na kuisaidia timu kushinda, na hilo ndilo limenileta hapa Simba,” aliongeza.
Usajili wa Sowah unaifanya safu ya ushambuliaji ya Simba SC kuonekana kuwa na nguvu zaidi kuelekea msimu mpya wa mashindano ya ndani na kimataifa, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kumuona akivaa jezi nyekundu kwa mara ya kwanza.