×

Dunia Uliyoiacha Nyuma – 56

Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.

Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.

Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.

Baadaye Magesa anagundua kwamba Grace ni jasusi wa kimataifa, akiwa amebadilisha jina na mwonekano wake, jambo linalompa hofu kubwa ndani ya moyo wake. Hata hivyo, msichana huyo anamuelewesha hali halisi.

Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi. Tayari baadhi ya mambo yameanza kufichuka ambapo inaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya kifo cha Mwampashi na Magesa.

Kaburi ambalo kila mtu anaamini kwamba ndipo alipozikwa Magesa, linafukuliwa na sampuli zinachukuliwa kwa ajili ya vipimo vya DNA. Baadaye inabainika kwamba aliyezikwa hakuwa Magesa bali mtu mwingine tofauti kabisa.

Kadiri upelelezi unavyozidi kupamba moto ndivyo mambo mengi yanavyozidi kuibuka na sasa watu wengine wanahojiwa kuutafuta ukweli wa tukio zima. Sekretari wa Magesa na yule wa waziri mkuu nao wanahojiwa ambapo mambo ya ajabu yanazidi kubainika na sasa ipo wazi kwamba kuna mkono wa waziri mkuu.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Haiwezekani! Mheshimiwa waziri mkuu hawezi kushiriki kwenye njama hatari kama hizi.”

“Kwa nini isiwezekane? Mpaka hapa ushahidi wote unaonesha kwamba yeye ndiye mtuhumiwa wetu namba moja.”

“Sasa hata kama ushahidi unaonesha hivyo, unafikiri tunayo mamlaka ya kumchunguza kweli? Na akijua kwamba tumeshajua si anaweza kutufanyia njama hata sisi wenyewe tukapoteza kazi zetu?”

“Kama tumeamua kuyavulia nguo maji, sharti tuyaoge. Huu woga wetu unatokana na nini? Hakuna ambaye yupo juu ya sheria,” maafisa watatu wa ngazi za juu katika idara ya usalama, Ephraim Mandiba, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usalama wa Taifa, Pius Kasekwa, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali na Inspekta Jordan Ngai, Mkuu wa Upelelezi, walikuwa wakijadiliana.

Baada ya kazi nzito waliyoifanya bila kupumzika, hatimaye mwanga wa kila kitu kilichokuwa kimejificha nyuma ya pazia ulianza kuonekana.

“Mimi nashauri jambo moja muhimu, inatakiwa tukusanye ushahidi wote muhimu ambao unaweza kumtia hatiani mheshimiwa moja kwa moja pamoja na watu wote walioshirikiana naye kwa sababu lazima tujue kwamba hajafanya haya yote peke yake.

“Baada ya hapo, tumshirikishe mwanasheria mkuu wa serikali na spika wa bunge na ofisi yangu ambazo kimsingi zinao uwezo wa kikatiba wa kutengua kinga ya kutoshtakiwa ya kiongozi yotote kisha baada ya hapo afunguliwe mashtaka,” alisema mwendesha mashtaka mkuu wa serikali, Pius Kasekwa huku akionesha kukosa amani ndani ya nafsi yake.

“Jamani nasisitiza tena, hakuna haja ya kuogopa chochote, ni bora kufa tukiwa tumesimama kuliko kuishi tukiwa tumepiga magoti, hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria.

“Nawahakikishia kwamba hakuna jambo linaloweza kutuletea heshima kubwa kama tukilisimamia suala hili kwa haki na kuhakikisha wote waliohusika, wakiongozwa na mheshimiwa waziri mkuu wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usalama wa Taifa, Ephraim Mandiba akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara.

*    *    *

“Mossad agent! ID code Bravo, Chali, Chali 761! Requesting permission to access your database! (Afisa wa Mossad! Namba ya utambulisho BCC761! Naomba ruhusa ya kuingia kwenye mfumo wenu wa kompyuta) sauti ilisikika kwenye kompyuta kubwa iliyokuwa ndani ya chumba cha kuongozea mitambo ya ulinzi (control room) makao makuu ya jeshi la polisi! Ikasikika mara ya kwanza, ikarudia tena mara ya pili na hatimaye ikasikika kwa mara ya tatu! Huo ndiyo ulikuwa utaratibu wa kimataifa wa jinsi majasusi walivyokuwa wanawasiliana, bila kujali nchi wanazotoka.

Taa ndogo nyekundu zilizokuwa zimeunganishwa na kompyuta hiyo zikawa zinawakawaka na kuzima huku mlio fulani ukisikika.

Askari aliyekuwa zamu, Edwin Mulisa ambaye pia alikuwa mtaalamu wa kuongoza mitambo ya ulinzi zikiwemo kamera za CCTV, vinasa sauti na mawasiliano ya intaneti yaliyokuwa yameunganishwa moja kwa moja na satelaiti ya usalama iliyokuwa inatumika na jeshi, alibonyeza kitufe fulani kwenye kompyuta hiyo kisha akaanza kuzungumza na yule mtu.

“Hotel Quebec 666! Hotel Quebec 666! Hotel Quebec 666! Your registration number!” (HQ 666! HQ 666! HQ 666! Taja namba yako ya usajili)

Baada ya swali hilo, upande wa pili ulisikika ukitaja namba za siri huku yule askari mtaalamu wa kompyuta akiziandika kwenye laptop yake. Haikuwa kawaida kupokea maombi ya kimataifa kama hayo, tena kutoka kwa mashirika makubwa ya kijasusi kama  Mossad! Akawa anafanya kazi kwa kasi kubwa!

Alipomaliza kuingiza zile namba, alibonyeza kitufe kwenye laptop hiyo kilichoandikwa ‘Enter’, skrini kubwa iliyokuwa ukutani ikafunguka kisha ikaonekana sura ya mwanamke akiwa amevalia nguo za kijeshi, begani akiwa na nyota kadhaa huku ikiwa na maelezo yote muhimu, ikiwemo jina, mahali alipokuwa pamoja na vyeo vyake ndani ya Mossad!

“Mungu wangu, kuna nini tena?” alisema Mulisa huku akinyanyua simu ya mezani na kubonyeza namba fulani kisha akasogeza mkonga sikioni huku akionesha kuwa na wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wake.

“Hotel Quebec 666! Hotel Quebec 666! Hotel Quebec 666! Sir! Agent from Mossad is trying to access our database!” (HQ 666! HQ 666! HQ 666! Mkuu, jasusi kutoka Mossad anaomba ruhusa ya kuingia kwenye mfumo wetu wa kompyuta) alisema Mulisa na muda mfupi baadaye, mlango wa chumba alichokuwemo ulifunguliwa, maafisa wawili walioonesha kuwa ni wa ngazi za juu ndani ya jeshi kutokana na jinsi walivyovaa, waliingia harakaharaka na kuisogelea ile skrini kubwa iliyokuwa ukutani.

“Anasemaje?”

“Bado hajazungumza chochote zaidi ya kuomba ruhusa.”

“Hebu mruhusu kisha muweke kwenye conference call!” alisema mmoja kati ya wale wanaume, Mulisa akabonyeza laptop yake harakaharaka na muda mfupi baadaye, video iliyokuwa inamuonesha ‘live’ mwanamke huyo ilikuwa ikionekana.

“Access Granted! Welcome! What can we help you?” (Umeruhusiwa! Karibu, tukusaidie nini?)

“May I speak in Swahili please!” (Naomba niongee kwa Kiswahili tafadhali) alisema mwanamke huyo kisha akabadili lugha na kuanza kuzungumza Kiswahili fasaha, jambo lililowafanya wote waliokuwa ndani ya chumba kile kutazamana.

“Najua mnaendelea na uchunguzi kuhusu sakata la Magesa na Mwampashi. Naomba mniunganishe na wanaohusika na uchunguzi wa sakata hilo, ninao mchango muhimu wa kuwapa,” alisema mwanamke huyo, wote wakatazamana tena.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne ijayo kwenye Gazeti la Uwazi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

1 Comment

Leave a Comment