Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.
Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.
Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.
Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.
Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba wawili hao ni wapenzi.
Hatimaye wawili hao wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya. Mapenzi kati ya Arianna na Msuya yanaanza kukolea, jambo linalosababisha Diego awe kwenye wakati mgumu sana kihisia kutokana na wivu uliokuwa ukimsumbua kila kukicha.
Asubuhi moja, Msuya anaondoka kuelekea kazini lakini huku nyuma, Arianna na Diego wanakutana kama kawaida yao. Baadaye Msuya anagundua kwamba amesahau kitu nyumbani kwake.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Msuya alipoondoka tu, Diego aliyekuwa akichungulia kupitia dirisha la chumbani kwake, alitoka na kuelekea chumbani kwa Arianna. Msuya akiwa anakaribia kufika ofisini kwake, alikumbuka kwamba kuna kitu cha muhimu sana amesahau nyumbani kwake, harakaharaka akageuza gari na safari ya kurudi nyumbani kwake ikaanza.
Kwa kasi kubwa, gari la kisasa aina ya Chevrolet Trailblazer lilikuwa likikatiza mitaa kuelekea nyumbani kwa Msuya huku mwenyewe akijitahidi kuongeza kasi ili awahi kufika na kurudi kazini bila kuchelewa.
“Hivi kwa nini nisimpigie simu Arianna na kumpa maelekezo ya ninachokitaka ili nikifika tu getini aniletee?” aliwaza Msuya, harakaharaka akachukua simu yake na kuanza kutafuta namba ya Arianna na muda mfupi baadaye, tayari simu yake ilikuwa hewani.
Cha ajabu simu hiyo iliita mpaka kukatika bila kupokelewa, jambo ambalo halikuwa kawaida ya Arianna. Msuya hakuchoka, alipiga tena lakini bado hali ilikuwa ni ileile, akaamua kuiweka simu pembeni na kuendelea na safari.
***
“Vipi Diego? Mbona mbiombio kiasi hicho.”
“Nimekumiss mpenzi wangu, yaani nilikuwa naona kama huyo bwege wako anachelewa kuondoka. Si unajua nilishazoea kulala na wewe kitanda kimoja mpaka asubuhi, siku hizi nauona usiku unakuwa mrefu kweli,” alisema Diego huku akimvamia Arianna mwilini na kuanza kumbusu huku na kule.
“Mh! Taratibu basi, papara za nini,” alisema Arianna huku akijitahidi kujitoa kwenye mwili wa Diego kwa sababu ndiyo kwanza alikuwa ametoka kuamka hivyo hakupata japo muda wa kujimwagia maji kwanza.
“Diego mbona hunielewi? Taratibu basi, mimi ni wako haraka za nini?” alisema Arianna, safari hii kwa sauti iliyobeba ujumbe zaidi. Akamtaka kijana huyo amsubiri aende kupiga mswaki na kuoga kwanza kisha ndiyo mambo mengine yatafuatia.
“Mbona siku nyingine nilikuwa naenda kukuogesha? Twende na leo nikakuogeshe.”
“Hapana Diego, unajua tuko ndani ya nyumba ya watu, mwenyewe akishtukia hujui anaweza hata kutupiga risasi?”
“Usiogope Arianna, ameshaondoka na hapa kurudi ni mpaka jioni,” alisema Diego, bila hata kusubiri Arianna atamjibu nini, alivua fulana aliyokuwa amevaa kisha akavua na suruali, akabaki na bukta yake, akatangulia bafuni.
Mapigo ya moyo yalikuwa yakimuenda mbio sana Arianna, alijua madhara ya walichokuwa wanakifanya lakini kwa sababu Diego alikuwa na kawaida ya kung’ang’ania jambo, aliamua kumfurahisha ili mambo yaishe.
Akavua nguo alizokuwa amevaa na kuzitupa kitandani, juu ya nguo za Diego kisha akajifunga taulo juu kidogo ya kifua chake na kuelekea bafuni.
“Nimemisi sana kuwa karibu na wewe kama hivi,” alisema Diego huku akimvuta Arianna kwenye bomba la ‘mvua’, wakaanza kuogeshana kwa mahaba kama ilivyokuwa siku za mwanzo wakati wanaanzisha uhusiano wa kimapenzi.
Wakiwa kwenye hali hiyo, Arianna alishtuka kusikia simu yake inaita mfululizo, akajua lazima atakuwa ni Msuya anampigia kwani hakukuwa na mtu mwingine aliyekuwa akiwasiliana naye.
“Simu yangu inaita ngoja nikapokee.”
“Nani anakupigia saa hizi? Hakuna kwenda, huu ni muda wangu wa kuwa na wewe.”
“Diego, niache nikapokee simu bwana!”
“Nimeshakwambia huu ni wakati wangu, sitaki ukapokee,” alisema Diego huku akionesha kumaanisha alichokisema, Arianna akakosa cha kufanya zaidi ya kutulia.
Simu ilianza tena kuita lakini Arianna hakwenda kuipokea, ikaita mpaka ilipokata.
akiwa wanaendelea kuogeshana, wote walishtuka mno baada ya kusikia honi ya gari ikipigwa getini, wakajua lazima ni Msuya amerudi.
“Si nilikwambia wewe, unaona sasa?”
“Mungu wangu, nimekwisha,” alisema Diego huku akivaa bukta yake harakaharaka, akatoka bafuni mbio mpaka chumbani kwa Arianna ambako alichukua nguo zake na kutoka mbio mpaka nje huku akiwa makini kuhakikisha hakuna anayemuona.
Alipofungua mlango wa chumba chake na kuingia tu, tayari geti lilikuwa limeshafunguliwa, gari la Msuya likaingia mpaka kwenye maegesho.
“Mbona nakupigia simu hupokei kipenzi changu?” Msuya alimuuliza Arianna kwa upole baada ya kuingia ndani.
“Nilikuwa naoga mume wangu, nisamehe sana,” alisema Arianna huku hofu kubwa ikishindwa kujificha usoni mwake. Kama Msuya angemtazama vizuri, lazima angegundua kwamba kuna jambo lakini kwa sababu ya haraka alizokuwa nazo, hakumchunguza vizuri.
“Kuna ‘bussiness card’ muhimu sana nimeisahau, nilitaka ukaichukue chumbani kwangu ili nikija niishie getini lakini ndiyo ukawa unaoga, basi usijali nimesharudi,” alisema Msuya, akapanda ngazi harakaharaka mpaka chumbani kwake, akachukua alichokifuata kisha akashuka na kumuaga Arianna.
Ni mpaka gari la Msuya lilipoondoka ndipo Arianna aliporudi kwenye hali yake, akashusha pumzi ndefu na kuinua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu wake. Diego aliendelea kutulia chumbani kwake kwa muda mrefu mpaka baadaye sana ndiyo akatoka na kumfuata Arianna chumbani kwake.
Kama kawaida yao, walijidunga madawa ya kulevya, wakafanya mapenzi kisha Diego akatoka na kumuacha Arianna akiwa amelala fofofo.
Je, nini kitafuatia? Usikose kufuatilia Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.