Bado niko kwenye muendelezo wa aina za magonjwa yanayohusiana na mwanamke kupata muwasho na kutokwa na majimaji ukeni ambapo wiki iliyopita nilianza kuuzungumzia ugonjwa wa Trikomonia. Niliishia kuzungumzia dalili za ugonjwa huo.
KINGA YA UGONJWA
Ni kujiepusha na ngono zembe, kujitibu na kumtibia mpenzi wako. Ugonjwa huu unafanana na magonjwa ya Klamidia, yutiai na ‘PID’ au maambukizi katika viungo vya uzazi.
MADHARA
Madhara ya Kisonono ni katika mirija ya uzazi ambayo huweka usaha, huvimba, huweka makovu na hatima yake ni ugumba. Pia Kisonono kikipona husababisha mwanamke apate mimba nje ya kizazi, yaani kwenye mrija hapa mimba inakulia ndani ya mrija ambapo athari zake ni mrija kupasuka.
USHAURI
Mgonjwa atafanyiwa vipimo mbalimbali kama mkojo, vipimo vya ukeni na vile ambavyo daktari ataona vinafaa. Matibabu na uchunguzi hufanyika katika Hospitali za mikoa.
UGONJWA WA KLAMIDIA
Ugonjwa huu huambatana na kutokwa na majimaji machafu ukeni yenye harufu ni majimaji mazito. Majimaji haya pia huathiri njia ya mkojo.
JINSI TATIZO LINAVYOTOKEA
Ugonjwa husababishwa na vijidudu viitwavyo ‘Chlamydia Trachomatis’. Ni tatizo linalowapata watu walio na umri chini ya miaka 25, watu wenye kipato cha chini na wenye wapenzi wengi.
DALILI ZA UGONJWA
Mwanamke huanza kulalamika kutokwa na majimaji mazito ukeni yenye harufu mbaya bila muwasho, baada ya muda hupatwa na maumivu ya tumbo chini ya kitovu kuzunguka kiuno. Lakini katika hatua za awali hana maumivu hata historia ya ngono huwa ya muda mrefu zaidi ya miezi mitatu nyuma.
KINGA
Mwanamke katika hatua za awali hana dalili zozote hivyo hawezi kujua kama ameambukizwa kwa hiyo ni vema kuepuka ngono zembe na kuhakikisha unajitibu mapema pamoja na mpenzi wako. Uchunguzi wa mara kwa mara ufanyike hasa vipimo vya ukeni kuona kama kuna maambukizi na hasa kwa wanawake wanaotafuta ujauzito kwani ndiyo huathirika zaidi na tatizo hili.
MADHARA
Ugonjwa huu huathiri viungo vya ndani vya uzazi vya mwanamke na kuziba mirija ya uzazi hivyo mwanamke kuwa mgumba. Tatizo lingine ni kupata mimba nje ya kizazi.
Maambukizi kwa mjamzito husababisha kuzaa mtoto kabla ya muda wake. Maambukizi haya katika viungo vya uzazi vya mwanamke yana uwezo wa kukaa miaka mingi.