×

Sababu 5 za kukubali maumivu ili uwe na furaha!

Kuhangaikia furaha ndiyo sababu ya wengine kuumia na kutafuta ushauri wa hapa na pale kwa wataalam wa saikolojia na maisha.

Kuna watu wameamua kuitafuta furaha kwa kila njia ndiyo maana wapo wanaofikia hatua ya kuua, kuiba au kufanya mambo mengine ya ajabu wakiamini watapata furaha.

Wakati mwingine kuhangaika sana bila mafanikio kunaweza kukusababishia unyonge, wengine hujikuta wanapata mfadhaiko, hujikuta wakichanganyikiwa bila kujua kuwa maumivu wakati mwingine huja ili wapate furaha ya maisha.

Wapo watu ambao hawajui jinsi ya kuwa na furaha, wanapopatwa na jambo baya huendelea kulalamika na kumlaumu Mungu kwa kumpa mtihani fulani ambao umemsababishia kukosa furaha lakini wanashindwa kujua kuwa mwanzo wa huzuni ndiyo mwisho wa huzuni na ndiyo mwanzo wa furaha mpya.

Wengine hujikuta wakiwa na hasira mbaya kwa kukosa furaha, pengine hasira hiyo huwasababishia kujinyonga, kujichukia na hata kuwachukia watu pasipo na sababu.

Kama wewe ni miongoni mwa watu hao, unashauriwa kutokula vyakula vyenye kukupa hasira.

 Madaktari wanaohusika na vyakula wanajua hili, huwashauri watu kula vyakula vya kupoza hasira kwani hilo ndilo tatizo kubwa unapokuwa umekosa furaha katika maisha.

Wiki hii nimekuletea sababu 5 za kukufanya ukubali maumivu ili uweze kuwa na furaha;

  1. Maumivu yanakusaidia kukupa hamasa

Ukiwa na furaha wakati wote huwezi kujitambua kuwa una furaha, unatakiwa kupata uzoefu wa kitu tofauti, yaani maumivu kidogo ili ujifunze.

Maumivu hukupa hamasa ya kufanya jambo fulani kubwa ili kuondoa ile hali ya kushindwa. Kwa mfano mtu anakudharau hadharani kuwa huwezi jambo fulani, kile kitendo kikikuuma lazima utafanya kila njia ili umuoneshe mtu kuwa unaweza, hapo ndipo hamasa hukujia.

  1. Maumivu yakiondoka unapata furaha zaidi

Ukijiona umepata nafuu na maumivu yameondoka utajikuta ni mwenye furaha mara mbili na utasahau kila kilichotokea hapo nyuma. Wachunguzi wa mambo wanasema kuwa, maumivu yakiondoka unajikuta umejifunza kitu kutokana na yale maumivu, kiwango cha furaha huongezeka.

Mfano; ukifukuzwa kazi sehemu kwa mara ya kwanza utaumia sana, yale maumivu yatakufanya utafute kazi kwa nguvu na ukiipata utaifanya kwa bidii sana, bidii uliyonayo ndiyo mwanzo wa furaha ya milele.

  1. Maumivu hukuunganisha na watu

Kuna watu wengi wakiwa makazini au sehemu ambayo anajiona ana amani na furaha huwa ni ngumu kukutana na watu, lakini siku ukiwa na maumivu ni rahisi kujichanganya na watu ili tu kusahau matatizo yako, kukutana huko kunaweza kukusaidia ukajikuta unaongeza kitu kikubwa kwenye akili yako. Pia unaweza kujikuta unapata uzoefu wa mambo ambayo ulikuwa huyajui.

  1. Maumivu yanakupa nafasi ya kujizawadia

Baadhi ya watu wanapokuwa na maumivu hupendelea kwenda sehemu kama za supermarket, maduka makubwa ambako atajinunulia vijizawadi kama vile chokleti, pipi nk. Wenye tabia hii wengi wao ni wanawake.

Zawadi hizo za vitu vitamtamu kisaikolojia ni dawa kwa wakati mwingine kwani sukari yake husaidia kuondoa maumivu.

  1. Maumivu yanakufanya uwe muangalifu

Mara nyingi mwanadamu ukipata maumivu hujikuta unakuwa mwangalifu ili maumivu hayo yasirudi tena, unaweza kuhakikisha unafanya kila njia kwa umakini mkubwa.

Wafanyabiashara wengi waliotoka kwenye umaskini na kuwa matajiri hulinda sana heshima yao ya kuitwa matajiri kwa kufanya kazi kwa bidii, kwani huogopa maumivu waliyowahi kuwa nayo.

Mwisho naweza kukwambia kuwa, usiogope  maumivu. Kuna msemo unaosema: “Maumivu huwa hayategemewi na kuumia ni kuamua.”

Leave a Comment