×

Jini Mauti-25

Ilipoishia wiki iliyopita

Kifo cha Hemedi kilinitisha mno achilia mbali kuniumiza, nikawa najiuliza kwa nini hakunielewa nilipomkataza na kumweleza angefariki dunia.

“Wewe dada!” aliita msichana wa mapokezi, aliniita baada ya kuniona nikikimbia. Endelea nayo…

Sikutaka kuitikia, sikutaka kugeuka, niliendelea kusonga mbele, nikaufungua mlango na kukimbia zangu huku hata wateja waliofika katika gesti ile wakishangaa. Sikujua nini kiliendelea pale, niliondoka huku nikikimbia mpaka nyumbani.

Sijui kitu gani kilitokea ila nilihisi nishazoea mauaji yale kwani sikuwa nikilia tena, nilipofika nyumbani nikaingia chumbani huku macho yangu yakiwa makavu kabisa lakini nilikuwa na mawazo mno.

Mama hakuweza kugundua, nilijifanya mchangamfu kila nilipokutana naye. Kesho ilipofika, nikaelekea shuleni, stori zilizokuwa zimetapakaa ni juu ya dereva bodaboda, Hemedi aliyekutwa amekufa kule gesti.

“Mmmh! Nasikia kafa kifo kibaya sana,” nilimsikia mwanafunzi mmoja akimwambia mwenzake, nikasimama pembeni na kuanza kusikiliza kisiri.

“Kifo gani?”

“Kakutwa kakakamaa chumbani, mapovu yanamtoka, damu kila sehemu,” alijibu mwanafunzi huyo.

“Au alimchukua jini?”

“Basi najua! Sijui ilikuwaje,” alisema mwanafunzi huyo.

“Halafu si ndiyo nasikia alikuwa akimmendea mwanafunzi mmoja hapa!”

“Yupi?”

“Mmmh! Nilisikia tu juu kwa juu, sijui chochote kile,” alijibu mwanafunzi huyo.

Niliposikia maneno hayo, moyo wangu ukalia paaa, nikaona kwamba ingejulikana kwamba mimi ndiye niliyehusika katika mauaji hayo. Niliogopa sana, sikuamini kwamba japokuwa nilijitahidi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi wa siri na Hemedi watu wengine wangeweza kufahamu.

Nikaondoka na kuelekea darasani, amani ikatoweka moyoni mwangu, masikio yangu yakawa wazi kuwasikiliza watu wangesemaje kuhusu mimi. Hakika nilikuwa na hofu mno.

“Davina…” nilisikia nikiitwa, nikauinua uso wangu kuona alikuwa nani, aliyesimama mbele yangu alikuwa Michael, yule mwanafunzi wa kidato cha nne aliyekuwa akinifuatilia.

“Unasemaje?” niliuliza kwa hasira.

“Mbona upo hivyo?”

“Nipo vipi?”

“Mmmh! Hebu punguza hasira kwanza.”

“Nikusaidie nini?”

“Davina!”

“Si useme unasemaje!”

“Mbona unanitisha!”

“Nakutisha kwa lipi?”

“Punguza hasira kwanza.”

“Bwanaeee hebu nitokee huko,” nilisema kwa sauti kubwa, wanafunzi wote wakasikia, wakageuka kule nilipokuwa, Michael akanyong’onyea sana.

Michael akajisikia aibu, akabaki akiniangalia, akainamisha uso wake chini na kuanza kuondoka darasani humo. Nilikuwa nimechanganyikiwa mno, sikutaka kusikia la mtu yeyote yule, kitendo cha Hemedi kufariki kilinisikitisha mno.

Nilimwacha Michael aondoke lakini ukweli ni kwamba hata mimi mwenyewe nikaanza kumuonea huruma, alikuwa kijana mpole, hakustahili kukaripiwa, alikuja kwangu kwa ajili ya kunijulia hali tu lakini kutokana na hali niliyokuwa nayo, likatokea la kutokea.

Itaendelea wiki ijayo.

Leave a Comment