Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale sharobaro Nelly na rafiki ya Ipyana walipowasili Posta na kwenda moja kwa moja kwenye jengo la wizara moja ambapo Ipyana alikuwa akifanya ujasiriamali wa kuosha magari. Je, baada ya kuwasili hapo kilijiri nini? Songa mbele na utamu huu…
Hadi ilipofika saa tatu na nusu walikwishamaliza kuosha magari manne, kwa gharama ya shilingi 4,000 kwa gari moja na tayari walikuwa wana uhakika wa kupata shilingi 16,000.
“Umeona besti, haya magari manne tayari tuna uhakika wa kupata shilingi 16,000,” Ipyana alimwambia Nelly ambaye alimwambia aliamini ile kazi ililipa.
Wakati wakiwa wanapiga stori wamekaa eneo la kuoshea magari, alikuja dada mmoja wa idara ya uhasibu mwenye shepu matata sana, akawasalimia akina Ipyana.
“Sisi hatujambo da Fatu, vipi kazi?” Ipyana alimsabahi.
Dada huyo ambaye kwa jinsi alivyoumbika na nguo alizovaa kumkaa sawa, Nelly akajikuta anameza tu mafunda ya mate na kujisemea moyoni kwamba wakubwa walikuwa wanafaidi sana.
“Vipi Ipyana, naona leo umetuletea mwenzako, kazi zinakuzidi nini?” Fatu alimwuliza Ipyana kabla hajamweleza shida yake.
“Nimeamua tu kuja na ndugu yangu maana nimeona yupoyupo tu homu,” Ipyana alimwambia.
“Vizuri sana na huo ndiyo urafiki wa kweli, anaitwa nani?” Fatu alimwuliza dada huyo aliyeonekana kuvutiwa na kitu f’lani kwa sharobaro Nelly.
“Nelson, ila wengi wanapenda kumuita jina lake kwa kifupi yaani Nelly,” Ipyana akamwambia.
“Oke, karibu sana Nelly, tena kwa kuwa leo ndiyo mara yako ya kwanza kufika hapa nataka gari langu ulioshe wewe, nitakupa shilingi elfu sita kama ofa ya kukukaribisha,” Fatu alimwambia Nelly, kijana huyo ambaye hakuamini alichokisikia akasema asante.
“Leo Ipyana ni zamu ya rafiki yako mgeni, wewe umekula sana hela zangu, sasa gari langu lile pale nataka kuona rafiki yako atakavyoling’arisha,” Fatu alimwambia Ipyana.
“Dada Fatu bwana kwa visa, haya bwana wewe kaendelee na kazi lakini elewa wadogo zako bado hatujanywa chai,” Ipyana akamtania.
“Kwani mimi ndiye nimewaleta mjini, mtakula jeuri yenu,” Fatu alimtania Ipyana kisha akaingiza mkono kwenye sketi yake iliyombana na kutoa noti ya shilingi 5,000 akampatia Ipyana.
Ipyana na Nelly walimshukuru ndipo dada huyo akaenda kuendelea na kazi, hata hivyo alivutiwa sana na muonekano wa Nelly ambaye alikuwa mrefu wa wastani, maji ya kunde, ana vidiponsi vilivyomfanya anapotabasamu au kucheka vionekane.
“Ukiwa na kijana kama huyo mbona ni raha tupu siyo kama mzee wangu hajiwezi kabisa eneo la kujidai, huyu nitafanya kila njia nimpate,” Fatuma ambaye wengi walipenda kulikatisha jina lake aliwaza.
“Kaka umeona mambo ya Posta hayo? Mpaka muda huu tayari tuna shilingi 21,000 hata saa tano haijafika, halafu una nyota ya kupendwa, si umemuona dada Fatu alivyokuchangamkia na kutoa hela ya chai?” Ipyana alimwambia Nelly.
“Siyo mchezo kaka, halafu dada yupo bomba mbaya, kweli wakubwa wanafaidi da!” Nelly alimwambia Ipyana.
“Siyo wakubwa, hata wewe ukiamua kujitosa mazima unachukua mzigo, hawa madada wa maofisini huwa wanawapenda sana vijana kama sisi,” Ipyana alimwambia Nelly.
“Acha kunitania Ipyana, dada kama yule mwenye hela zake na alivyo vile anaweza kutoka na vijana kama sisi tusio na mbele wala nyuma?” Nelly alimwuliza rafiki yake.
“Kwani unafikiri wana tofauti gani na mtoto wa kishua aliyekupa hadi simu, mapenzi hayanaga sera hizo ni sawa na kipepeo asiyechagua ua la kutua,” Ipyana alimwambia Nelly.
Nelly alifurahishwa na kauli ya Ipyana na kujikuta akicheka na kumwambia hakujua kama alikuwa na maneno mengi namna ile, rafiki yake huyo alimwambia kauli yake ilikuwa kweli tupu!
Kabla hata hawajaenda lilipokuwa gari la Fatuma, alitokea dada mwingine mfupi wa wastani, mweusi wa kung’aa, nyuma ana kiwowowo cha kuleta fujo mjini, miguu ya bia, macho makubwa akikutazama ni kama vile anakukonyeza na midomo f’lani hivi ya mahaba.
Kwa tabia ya kupenda wanawake kuliko hata chakula, Nelly alipomuona tu moyo ukapiga paaa!
Je, baada sharobaro Nelly kupatwa na hali hiyo kilifuatia nini? Tafadhali usikose utamu huu wiki ijayo.
Maoni tumia namba hiyo juu.