ILIPOISHIA IJUMAA:
Nikacheka kidogo kabla ya kumuuliza:
“Wewe unataka ninywe bia?”
“Ndiyo.”
Mzungu akaagiza mzinga wa pombe kali mimi akaniagizia pombe ya kawaida.
Mhudumu alipoondoka, mzungu huyo aliniambia alikuwa amefurahi kuwa na mimi siku ile. Alinitajia sehemu mbalimbali ambazo alisema aliwahi kuniona kabla ya siku ile na akanipenda.
Sehemu alizonitajia ilikuwa ni kweli niliwahi kufika. Hapo nikajua kuwa kukutana kwetu hakukuwa kwa bahati tu bali alikuwa akinifuatilia.
Mazungumzo yetu hayo yalikatizwa wakati yule mhudumu alipotuletea vileo tulivyoagiza.
SASA ENDELEA…
Wakati tunaendelea kunywa, Smith alinitamkia kuwa alikuwa amenipenda sana. Bila shaka ile pombe aliyokuwa anakunywa ndiyo iliyompa ujasiri wa kunitamkia maneno hayo waziwazi.
Kwa upande wangu nilikuwa nikichekacheka tu. Nikagundua kuwa mzungu huyo anapolewa anakuwa na maneno mengi sana na hana aibu ya kuzungumza.
Akataka na mimi nimtamkie kuwa nimempenda. Nikamwambia kuwa nimempenda.
Nilipomwambia hivyo akaanza kung’ang’ania aende na mimi nyumbani kwake akimaanisha kule hotelini alikokuwa akiishi.
“Tutakwenda siku nyingine siyo leo,” nikamwambia.
“Kwa nini isiwe leo?” akaniuliza huku akinitolea tabasamu.
“Leo sikupanga kuja kwako, nilipanga nije hapa tuzungumze.”
“Sasa utakuja lini?”
“Kwani wewe huna mke?” nikamuuliza.
Smith akatikisa kichwa.
“Mke wangu utakuwa wewe.”
“Huko kwenu London huna mke?”
“Sina.”
“Una maana hujaoa bado?”
“Bado.”
“Kwa nini?”
“Mimi nataka mke wa Kiafrika kama wewe.”
“Na hapa Dar huna msichana mwingine?”
Simith akatikisa kichwa.
“Bado sijampenda yeyote zaidi yako.”
Wakati tunazungumza nilikuwa ninakunywa ile bia taratibu huku nikimtazama mzungu huyo na kupima maneno yake.
Ingawa nilimtamkia kuwa nampenda lakini sikuwa nimeshafanya uamuzi wa kuwa naye kwa harakaharaka vile.
“Utakuja lini nyumbani kwangu?” akaniuliza tena baada ya kupita ukimya mfupi.
“Nitakwambia.”
Jibu langu hilo likaufanya uso wake ufadhaike.
“Sikiliza. Naona bado hujaniamini lakini mimi ni mtu wa ukweli. Nitahakikisha kuwa maisha yako yanakuwa ya furaha utakapokuwa na mimi. Nitakununulia nyumba, nitakununulia gari na kama utanizalia mtoto nitakupeleka kwetu ukaishi huko na utakuwa kama malkia wangu.”
Maneno yake yalianza kunitia tamaa. Nikaanza kufikiria kuachana na mpenzi wangu Eddie, Mzanzibari aliyekuwa akisoma huko Uingereza ambaye tulipanga kuja kuoana atakapomaliza masomo yake.
Wakati namuwazia mzungu huyo niliona akitia mkono kwenye mfuko wa suruali yake akatoa burungutu la noti. Akaniambia:
“Chukua.”
Nikanyoosha mkono wangu na kulichukua lile burungutu.
“Ni milioni kumi,” akaniambia na kuongeza:
“Utakwenda kuzihesabu nyumbani. Tia kwenye mkoba wako.”
Sikupenda kudhihirisha usoni kwangu ni kwa jinsi gani nilifurahi. Nikafungua mkoba wangu na kuzitia pesa hizo.
“Okey. Nenda kafikirie, ni siku gani utakuja kwangu kisha utaniambia.”
“Sawa. Nitakwambia kwenye simu,” nikamwambia haraka.
Nilikunywa bia moja tu, sikutaka kuongeza nyingine. Nilihisi mazungomzo yangu na yule mzungu yalikuwa yamefikia tamati. Baada ya kupata zile pesa sikutaka kukaa tena pale. Nikamwambia:
“Mimi nakwenda zangu.”
“Hutaki kuongeza bia?” Smith akaniuliza huku akitoa tabasamu laini. Tabasamu lake lilikuwa kama la kunicheka mimi nilivyotaharuki baada ya kunipa zile pesa.
“Basi imetosha. Mimi silewi sana. Huwa nakunywa bia moja tu.”
Smith hakusema kitu, akabaki kunitazama huku akiendelea kutabasamu.
Nikainuka kwenye kiti na kuchukua mkoba wangu ambao niliutundika begani.
Smith naye akainuka.
“Sikiliza nikuambie kitu,” akaniambia. Alinyamaza kidogo kisha akaendelea.
“Ukija kwangu nitakupa zawadi nzuri sana na hutaisahau maishani mwako.”
“Nimekusikia. Usijali Mr Smith, tutakuwa pamoja. Kwa sasa acha niende kwanza. Lakini tutaongea mengi kwenye simu.”
“Sawa. Hakuna tatizo lakini nakuomba uzingatie niliyokwambia.”
“Nimeshayazingatia. Usijali.”
Nikaondoka. Smith akarudi kwenye kiti na kuendelea kunywa pombe yake.
Nilikodi teksi iliyonirudisha nyumbani. Wakati wote nikiwa kwenye teksi hadi nafika nyumbani, yule mzungu alikuwa ametawala akili yangu.
Zile milioni kumi alizonipa pamoja na maelezo yake mengine yakiwemo yale aliyonieleza kuwa nikienda huko hotelini anakokaa atanipa zawadi ambayo sitaisahau maishani mwangu, yalikuwa yamenihamasisha.
Je, nini kiliendelea? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.